Makala ya 13 ya fainali za Kombe la mataifa ya Afrika kwa wanawake yataanza kutifua vumbi leo Jumamosi usiku na kukamilika Julai 26, nchini Morocco yakishirikisha mataifa 12.
Timu 30 tofauti zimefuzu tangu kuanzishwa kwa kipute hicho mwaka 1998, huku Nigeria, ikijivunia kutwaa mataji 9,ikifuatwa na Equitorial Guinea, kwa mataji mawili nayo Afrika ikatawazwa mabingwa mwaka 2022 katika makala ya mwisho.
Katika fainali za mwaka huu Wenyeji Morocco, watafungua ratiba dhidi ya Zambia, kuanzia saa tano usiku katika mechi ya kundi A,kabla ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo kupambana na Senegal Jumapili Julai 6.
Kundi B linajumuisha Nigeria,Tunisia,Botswana na Algeria wakati mabingwa watetezi Afrika Kusini wakiwa kundi C pamoja na Ghana,Mali na Tanzania.
Viwanja vitano vilivyo katika miji mitano vitatumika kuandaa mechi hizo 24 vikiwa;El Bachir mjini Mohammedia,Larbi Zaouli na Perejego mjini Casablanca,Honneur mjini Oudja,Berkane na Olympic mjini Rabat.
Mechi zote zitarushwa mubashara kupitia runinga ya taifa ya KBC Channel 1.