Moshi mweusi ulifuka jana usiku kutoka wa dohani la Vatican, kuashiria kutokubaliana kwa Makadinali kwenye raundi ya kwanza ya upigaji kura wa kumchagua Papa Mtakatifu mpya wa Kanisa Katoliki.
Maelfu ya waumini wa Katoliki walisubiri kwa saa kadhaa nje ya makao makuu ya Kanisa Katoliki wakati wa upigaji kura huo hadi walipoona moshi mweusi.
Makadinali wa Katoliki 133 kutoka mataifa 90 duniani waliingia faraghani jana mjini Vatican kuanza shughuli ya kupiga kura kumtafuta Papa akayemrithi marehemu Papa Francis, aliyezikwa tarehe 27 mwezi uliopita baada ya kufariki akiwa na umri wa miaka 88.
Raundi ya pili ya upigaji kura inatarajiwa kupigwa leo, ambapo ikiwa thuluthi mbili ya makadinali hao watakubaliana, basi moshi mweupe utafuka kwenye dohani la Vatican.
Makadinali hao ambao wengi wao waliteuliwa na marehemu Papa Francis wametenga siku tatu za upigaji kura huku wakitarajiwa kukubaliana aidha leo au kesho.