Mahakama Kuu imetupilia mbali kesi iliyopinga uteuzi wa Mwenyekiti na Makamishna sita wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC).
Hata hivyo, kwenye uamuzi uliotolewa siku ya Alhamisi jioni, Mahakama hiyo iliharamisha ilani iliyotolewa na Rais William Ruto kwenye gazeti rasmi la serikali toleo la Juni 10, 2025 kuwateua makamishna hao.
Uamuzi huo uliotolewa na Majaji watatu wanaojumuisha Lady Justice Roselyne Aburili, Justice John Chigiti na Justice Bahati Mwamuye, ulisema kuwa licha ya kwamba uteuzi wa makamishna hao haukukiuka katiba, uchapishaji wa majina yao kwenye gazeti rasmi la serikali ulikiuka maagizo yaliyopo ya mahakama.
“Afisa mteule hawezi kula kiapo kupitia uteuzi haramu. Ili kuzingatia mfumo wa sheria, mchakato haramu hauwezi kuwa msingi wa uhalali wa IEBC,” walisema Majaji hao.
Huku ikitupilia mbali kesi hiyo, mahakama hiyo ilisema hakukuwa na ushahidi kuhusu madai ya mapendeleo, ukosefu wa uwakilishi sawa wa kimaeneo na ukosefu wa ushiriki wa umma.
Wawasilishaji wa kesi hiyo, walidai kuwa uteuzi wa mwenyeiti na makamishna haukuzingatia utaratibu ufaao na watu wanaoishi na ulemavu na wale wa makundi yaliyotengwa waliachwa nje.
Aidha, majaji hao walidokeza kuwa ipo haja kwa Bunge la Taifa kubuni sheria itakayotoa mwongozo kuhusu ushiriki wa umma kwenye masuala muhimu ya kitaifa kama vile kubuniwa kwa IEBC.
Uamuzi huo sasa unatoa fursa kwa Rais William Ruto kuwateua upya makamishna hao kupitia gazeti rasmi la serikali, ili waapishwe na kuanza kutekeleza majukumu yao.