Mahakama kuu yasimamisha usajili wa makurutu wa polisi

Marion Bosire
2 Min Read

Mahakama Kuu imesimamisha kwa muda, usajili uliokuwa umepangwa wa makurutu elfu 10 wa polisi, kufuatia kesi iliyowasilishwa na mtetezi wa haki za binadamu Eliud Matindi anayepinga usajili huo.

Uamuzi huu wa mahakama unajiri siku chache tu kabla ya tarehe ambayo usajili huo ungeanza kote nchini.

Jaji Bahati Mwamuye alitoa uamuzi huu leo Novemba 10, 2025, akielekeza kwamba ilani iliyotolewa ya usajili na Inspekta Jenerali wa polisi Novemba 4, 2025 iahirishwe hadi kesi hiyo isikilizwe na kuamuliwa.

Uamuzi wa leo unalenga wahusika wote wa kesi hiyo wakiwemo wafanyakazi, mawakala na mashirika yanayohusishwa na usajili wa makurutu wa polisi.

Mwasilishaji wa kesi hiyo alielekezwa awasilishe nakala za ombi lake na uamuzi wa mahakama kwa washtakiwa mara moja na kuthibitishia mahakama kwamba amefanya hivyo kufikia Novemba 12, 2025.

Washtakiwa kwenye kesi hiyo nao wanahitajika kuwasilisha majibu yao mahakamani kufikia Disemba 11, 2025, huku mwasilishaji akipata fursa ya kuwasilisha hoja zaidi kufikia Januari 9, 2026.

Kesi hiyo itatajwa tena Januari 22, 2026 kama njia ya kuthibitisha iwapo taratibu zimefuatwa na kujadili kuhusu kusikilizwa kulikoharakishwa kwa kesi hiyo.

Usajili wa makurutu wa polisi ulikuwa umepangiwa kuanza Novemba 17, 2025, na ungeandaliwa katika vituo 422 kote nchini kuanzia saa mbili asubuhi hadi saa 11 jioni.

Share This Article