Magonjwa yanayohusiana na baridi yaongezeka kufuatia kipindi kirefu cha baridi

Martin Mwanje
3 Min Read

Kenya inashuhudia ongezeko kubwa la magonjwa yanayohusiana na baridi kufuatia msimu wa baridi uliodumu kwa muda mrefu hadi mwishoni mwa mwezi Agosti 2025, hali isiyo ya kawaida kwa kipindi hiki cha mwaka.

Miezi ya Julai na Agosti imekuwa kilele cha baridi kali, huku maeneo ya Nairobi, Nyanda za Juu za Kati, na sehemu za Bonde la Ufa yakikumbwa na siku za mawingu, mvua nyepesi na joto la chini. Hali hii ya baridi imechangia ongezeko la maambukizi ya magonjwa ya mfumo wa upumuaji nchini kote.

Mnamo mapema mwezi Julai, Wizara ya Afya ilitoa tahadhari ikihimiza Wakenya kuchukua hatua za kujikinga dhidi ya magonjwa, kuvaa mavazi ya joto, na kuhakikisha kuwa nyumba zina hewa ya kutosha ili kupunguza kusambaa kwa maradhi ya kupumua.

Kwa mujibu wa wataalamu wa afya, hali ya baridi hupunguza uwezo wa mwili kujilinda dhidi ya magonjwa na kuwafanya watu wakae ndani kwa muda mrefu — mazingira yanayorahisisha kuenea kwa virusi.

“Hewa ya baridi hukausha na kupoza njia za hewa, na kusababisha mikazo ambayo hufanya iwe vigumu kwa mwili kutoa kamasi na uchafu mwingine,” alieleza afisa wa afya ya umma.

Ingawa mlipuko wa mafua ulioikumba nchi mwezi Mei umepungua, maafisa wa afya wanasema ongezeko la sasa la maambukizi linatokana zaidi na mafua ya kawaida na virusi vingine vinavyochochewa na baridi.

“Tunaloshuhudia sasa si mafua ya aina ya influenza, bali ni kuongezeka kwa visa vya mafua ya kawaida kutokana na baridi. Haya ni maambukizi ya virusi, na yanawaathiri watoto na watu wazima,” alisema Dkt. Albert Wagura Taiti, Waziri wa Afya wa kaunti ya Laikipia.

Aliongeza kuwa hali ya baridi pia inachangia kuzuka kwa magonjwa mengine kama vile nimonia na tonsilitis.

“Watu wanapaswa kuepuka kukaa karibu na mahali penye moshi, kwani moshi huleta muwasho na huchochea magonjwa ya kupumua. Pia, kukaa katika vyumba visivyo na hewa ya kutosha na vilivyolowa huchangia kuenea kwa virusi kutoka mtu mmoja hadi mwingine,” alisema Dkt. Taiti.

Aliwashauri wananchi kuepuka kutumia dawa bila ushauri wa daktari wanapopata dalili za mafua, na kusisitiza umuhimu wa tabia za kujikinga — hasa shule zinapofunguliwa wiki hii.

“Wazazi wanapaswa kuwajali zaidi watoto wanaorejea shuleni katika kipindi hiki cha baridi. Wahakikishe wamevaa nguo za joto, wanakunywa vinywaji vya moto, na wanazingatia usafi wa mwili. Ikiwa mtoto au mtu mzima ana mafua, kuvaa barakoa husaidia kupunguza maambukizi,” alieleza Dkt. Taiti.

“Tuweke afya na kinga mbele wakati huu. Baridi huenda isiweze kuzuilika, lakini magonjwa yanaweza kuzuiwa.”

Share This Article