Baraza la Magavana limeunga mkono mageuzi yanayotekelezwa na serikali ya kitaifa ya kukodisha kampuni za sukari kwa sekta ya kibinafsi.
Kupitia mwenyekiti wake Ahmed Abdullahi, Naibu mwenyekiti Mutahi Kahiga, na mwenyekiti wa kamati ya kilimo katika baraza hilo Ken Lusaka, Baraza hilo la Magavana lilitoa wito wa kukumbatiwa kwa mageuzi hayo kikamilifu.
Akizungumza mjini Mombasa leo Alhamisi wakati wa mkutano wa pamoja na Waziri wa Kilimo na Ustawi wa Mifugo Mutahi Kagwe, mwenyekiti wa baraza hilo Ahmed Abdullahi alitoa onyo dhidi ya kuingizwa siasa kwenye mchakato huo unaolenga kufufua sekta ya sukari hapa nchini.
Kwa upande wake Kagwe alitetea hatua ya kukodisha kampuni nne za sukari kwa muda wa miaka 30, akisema hatua hiyo itawanufaisa wakulima pakubwa pamoja na kuhakikisha huduma bora katika kampuni hizo za sukari.
Kagwe pia alishiriki mkutano na mawaziri wa kilimo kutoka kaunti zote 47 chini ya kauli mbiu ” Kuimarisha kilimo jumuishi kwa utoshelevu wa chakula na kuzalisha utajiri,”.