Magavana wajitenga na kauli za Mutahi Kahiga

Gavana Kahiga wa kaunti ya Nyeri amenukuliwa kwenye video moja akionekana kusherehekea kifo cha Waziri Mkuu wa zamani Raila Odinga.

Martin Mwanje
2 Min Read
Ahmed Abdullahi - Mwenyekiti wa Baraza la Magavana

Baraza la Magavana (CoG) limejitenga na matamshi ya Gavana wa Nyeri Mutahi Kahiga kuhusiana na kifo cha Waziri Mkuu wa zamani Raila Odinga. 

Kahiga alinukuliwa kwenye video moja ambayo imesambaa katika mitandao ya kijamii akionekana kusherehekea kifo cha Raila, wakati akihutubia hadhira katika eneo la Kieni.

Kwenye video hiyo, Kahiga anasikika akisema eneo la Nyanza lilikuwa likifaidika sana na miradi ya maendeleo, lakini kwa sababu Raila amefariki, eneo la Mlima Kenya sasa litafaidika.

Uhalisia wa video hiyo bado haujulikani wala Gavana huyo wa Nyeri hajatoa taarifa kuhusu kauli alizodaiwa kutoa kuhusu kifo cha Raila kwenye video hiyo.

Aidha, haijulikani nani aliyeirekodi video hiyo.

“Kama Baraza la Magavana, tungependa kujitenga kabisa na matamshi ya Gavana Kahiga na kuelezea kwamba hayo ni matamshi ya kibinafsi ambayo hayaakisi maoni ya Baraza la Magavana na hasa wakati huu wa maombolezo,” alisema mwenyekiti wa CoG Ahmed Abdullahi kwenye taarifa.

“Tunabaini kwamba matamshi hayo hakika ni ya kizembe, yasiyojali hisia za wengine, ya kuhuzunisha na kusikitisha. Ni ukosefu wa utu na haikubaliki kusherehekea kifo chake kwa misingi ya dhana ya miegemeo ya kisiasa. Mheshimiwa Raila Odinga alikuwa, na daima atasalia kuwa kiongozi shupavu ambaye michango yake imeandikwa katika historia ya nchi yetu. Hakuwa tu mwanzilishi na baba wa Ugatuzi lakini mtetezi na mfuasi wake mkuu.”

Abdullahi ambaye pia ni Gavana wa Wajir akisema amelazimika kuitisha kikao kisicho cha kawaida cha baraza hilo leo Jumatano asubuhi ili kuangazia matamshi yaliyotolewa na Gavana Kahiga.

Matamshi ya Kahiga yanajiri siku chache baada ya Raila aliyefariki Oktoba 15 kuzikwa nyumbani kwake huko Bondo Oktoba 19.

Viongozi wengi wa upinzani hasa kutoka Mlima Kenya hawakuhudhuria mazishi hayo.

Share This Article