Mafunzo kuhusu kukabiliana na ufadhili wa ugaidi na utakatishaji wa pesa kuzinduliwa

Mafunzo hayo yatatolewa katika hoteli ya Radisson Blu eneo la Upperhill jijini Nairobi Aprili 22 hadi 26, 2025.

Marion Bosire
2 Min Read

Jeshi la ulinzi la Kenya KDF kwa ushirikiano na muungano wa kiisilamu wa kijeshi kuhusu kukabiliana na ugaidi, linapanga kuzindua mpango ya mafunzo kuhusu kukabiliana na ufadhili wa ugaidi na utakatishaji wa pesa.

Kulingana na taarifa kutoka kwa jeshi la KDF, uzinduzi huo utafanyika katika hoteli ya Radisson Blu eneo la Upperhill jijini Nairobi Aprili 22 hadi 26, 2025.

Mafunzo hayo yanalenga kuimarisha uwezo wa kitaasisi na wa kibinafsi wa kukabiliana na taratibu za kifedha zinazosaidia ugaidi na uhalifu wa kupangwa.

Mkutano huo utawaleta pamoja wataalamu wa sheria, maafisa wa usalama na wadau wa kimataifa watakaoangazia teknolojia ya kisasa, mifumo ya kisheria na mikakati ya ushirikiano ya kuvuruga mitiririko haramu ya fedha.

Waziri wa ulinzi Soipan Tuya anatarajiwa kuongoza uzinduzi wa mpango huo wa mafunzo ambao unalenga pia kuhamasisha umma kuhusu hatari za kuchakata pesa na umuhimu wa hatua za kuzuia.

Muungano wa kiisilamu wa kijeshi kuhusu kukabiliana na ugaidi yaani Islamic Military Counter Terrorism Coalition (IMCTC), ni muungano wa ulimwengu ambao kwa sasa unahusisha nchi 42 ikiwemo Kenya.

Makao yake makuu ya muungano huo uliobuniwa Disemba mwaka 2015, yako jijini Riyadh nchini Saudi Arabia.

Lengo la kuanzishwa kwake ni kuratibu na kuunganisha juhudi za kukabiliana na ugaidi katika nchi wanachama kwa kuangazia vipengele kama vya kiitikadi, mawasiliano na ufadhili wa mipango ya kukabiliana na ugaidi.

Share This Article