Rais wa Venezuela, Nicolás Maduro, amesema yuko tayari kutetea uhuru wa taifa lake huku jeshi la Marekani likituma meli za kivita karibu na eneo la bahari la nchi hiyo.
Maduro alisema hakuna njia yoyote wanajeshi wa Marekani wanaweza kuvamia nchi yake, huku mvutano ukiongezeka kati ya Caracas na Washington,jeshi la wanamaji la Marekani likijikusanya Kusini mwa Caribbean, karibu na maji ya Venezuela.
Meli za kivita za Marekani zimefika katika eneo hilo kwa kile kinachoitwa operesheni dhidi ya magenge ya ulanguzi wa dawa za kulevya Amerika ya Kusini.
“Leo, tuko imara zaidi kuliko jana. Leo, tuko tayari zaidi kutetea amani, uhuru wa taifa, na mipaka yetu ya kitaifa,” alisema Maduro wakati akihutubia wanajeshi.
Maduro alitoa kauli hiyo wakati Balozi wa Venezuela katika Umoja wa Mataifa, Samuel Moncada, alikutana na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres, kulalamikia ongezeko la nguvu za kijeshi za Marekani katika eneo hilo.
“Hii ni operesheni kubwa ya propaganda ya kuhalalisha kile ambacho wataalamu wanakiita hatua ya kutumia nguvu za kijeshi – yaani uvamizi wa kijeshi katika nchi huru na inayojitegemea isiyo tishio kwa yeyote,” Moncada aliambia waandishi wa habari baada ya mkutano na Guterres.
“Wanasema wanatuma manowari ya nyuklia … yaani, ni jambo la kipuuzi kufikiria kuwa wanapambana na ulanguzi wa dawa za kulevya kwa kutumia manowari za nyuklia,” alisema balozi huyo.
Meli saba za kivita za Marekani na manowari moja ya nyuklia ya kushambulia kwa kasi, zilikuwa tayari katika eneo hilo au zilitarajiwa kufika katika wiki inayofuata, kwa mujibu wa afisa wa Marekani aliyezungumza na shirika la habari la Reuters kwa sharti la kutotajwa jina.
Zaidi ya wanajeshi 4,500 wa Marekani, wakiwemo wanamaji 2,200, waliripotiwa kuwa ndani ya meli hizo katika operesheni iliyoanzishwa baada ya utawala wa Trump kumtuhumu Maduro na viongozi wengine wa serikali yake kwa kuhusika na biashara ya dawa za kulevya aina ya cocaine.
Venezuela imejibu vitisho vya Marekani kwa kutuma meli za kivita na ndege zisizo na rubani kulinda pwani yake na kuzindua kampeni ya kuandikisha maelfu ya wanamgambo ili kuimarisha ulinzi wa ndani.