Maduka yapatayo 100 ya kuuza nyama yamefungwa na maafisa wa serikali katika eneo la Mbuzi Kata ya Murieti, jijini Arusha nchini Tanzania.
Wamiliki wa maduka hayo wanatuhumiwa kwa kutolipa ada hitajika kwa serikali na hivyo kujipata katika hatia ya kukiuka sheria za mamlaka za serikali.
Walioathirika walizua vurugu wakipinga vikali kufungwa kwa maduka yao hali iliyokwamisha biashara zao. Wafanyabiashara wanasema hawakupatiwa taarifa mapema na kwamba wanahitaji muda zaidi kurekebisha kasoro zilizotajwa.
“Kwa hivyo hatuelewi nini hasa kimejiri, tumekuta tu maduka yamefungwa, hatujapewa maelezo ya kina, hi imeathiri biashara zetu sana,” alisema mmoja wa Wafanyabiashara kwa masikitiko.
Licha ya juhudi za kupata taarifa rasmi kutoka kwa Mamlaka husika, hadi sasa haijafahamika bayana sababu kamili ya kufungwa kwa maduka hayo.
Wafanyabiashara hao wameiomba serikali kuingilia kati na kusaidia kurejesha hali ya kawaida kwa kufungua maduka na kuanzisha majadiliano ya haki baina yao na mamlaka.