Madereva watakiwa kuhakikisha magari yao yanakarabatiwa ili kupunguza ajali

Martin Mwanje
2 Min Read
Basi la shule lililohusika kwenye ajali Kisumu siku chache zilizopita na kusababisha vifo vya zaidi ya watu 20

Madereva wametakiwa kuhakikisha kuwa magari yao yanakarabatiwa ipasavyo na kuwa na vipuri halisi kama njia mojawapo ya kupunguza ajali nyingi ambazo zimekuwa zikitokea kwenye barabara mbalimbali humu nchini, hasa katika kipindi hiki cha mwezi wa Agosti.

Akizungumza katika eneo la Farm City kando ya barabara ya Isiolo–Meru wakati wa toleo la kwanza la Maonyesho ya Kibiashara ya North Connect, ambapo wananchi walielimishwa kuhusu mbinu za usalama barabarani na mashambani wanapotumia mashine mbalimbali kama trekta na mashine za kukatia nyasi, Meneja wa Shirika la Lewa Wildlife Conservancy, Dkt. John Kinoti ambaye alikuwa mgeni rasmi, alisema kuwa ajali nyingi husababishwa na magari ambayo hayajahudumiwa vizuri, jambo linalosababisha matatizo kama kushindwa kwa breki, huku uendeshaji mbaya pia ukitajwa kama chanzo kikuu cha ajali hizo.

Dkt. Kinoti pia alitoa wito kwa wamiliki wa magari kuhakikisha kuwa madereva wao wamepata mafunzo ya kitaalamu kutoka katika taasisi zilizosajiliwa, na madereva wa safari ndefu wapate muda wa kutosha wa kupumzika kabla ya kuanza safari.

Mwenyekiti wa Farm City, Stanley Kiambati, alisema kuwa shamba hilo kwa kushirikiana na Isuzu Kenya pamoja na Taasisi ya Fusion, walizindua kampeni inayojulikana kama “Macho Barabarani na Afya Njema” wiki iliyopita. Lengo kuu la kampeni hiyo ni kuwahamasisha madereva na wamiliki wa magari kuzingatia usalama kwa kuhakikisha magari yao yanahudumiwa mara kwa mara, na madereva wana mafunzo stahiki.

Aidha, alisisitiza umuhimu wa kutumia nishati mbadala kama vile nishati ya jua, pamoja na kuhamasisha matumizi ya magari na pikipiki za umeme kama njia ya kupunguza utoaji wa gesi chafu angani, hatua ambayo itasaidia kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.

Kiambati aliongeza kuwa maonesho hayo yatakuwa ya kila mwaka, ambapo wananchi watakuwa wakikutana kujifunza mbinu bora za kuongeza uzalishaji mashambani, huku vijana wakipewa nafasi ya kuonyesha vipaji vyao na kuviendeleza.

TAGGED:
Share This Article