Madereva wa matatu wandaa maombi Narok

Madereva hao walichochewa na visa vingi vya ajali ambavyo hushuhudiwa kwenye barabara ya Nairobi-Narok

Marion Bosire
2 Min Read

Madereva wa magari ya uchukuzi wa abiria almaarufu Matatu na polisi wa trafiki waliandaa maombi ya pamoja huko Mai Mahiu, kaunti ya Narok, kwenye barabara kuu ya kutoka Nairobi kuelekea Narok.

Dhamira ya hatua hiyo ni kutafuta uso wa Mungu kufuatia visa vingi vya ajali ambavyo hutokea kwenye barabara hiyo.

Madereva hao ambao wengi ni wa magari ya chama cha Narokline na wasimamizi wa kampuni hiyo waliandaa hafla hiyo ya maombi ambayo ilihudhuriwa na kamanda wa trafiki wa eneo hilo Patrick Leweri.

Mkurugenzi wa kampuni ya Narokline Andrew Mwangi alipongeza ushirikiano uliopo kati ya polisi wa trafiki na madereva katika kuhakikisha kanuni za trafiki zinazingatiwa.

Mwangi aliwataka madereva kuhakikisha kwamba magari yao yanatimiza viwango vinavyohitajika, ili kuepusha ajali zinazotokana na hitilafu za kimitambo.

Aliwaonya pia dhidi ya uendeshaji mbaya kama vile kupita magari mengine kiholela.

Kamanda wa kitengo cha trafiki huko Mai Mahiu Patrick Leweri alipongeza kampuni ya Narokline hasa madereva wake kwa kuongoza katika kuwa kielelezo kuhusu masuala ya usalama barabarani.

Alisema hatua yao ya kutafuta ulinzi wa Mungu wakiwa barabarani ndiyo njia bora huku akizitaka kampuni nyingine za uchukuzi wa abiria kuiga mfano wa Narokline katika kuafiki mahitaji ya usalama barabarani.

Leweri alionya pia dhidi ya mwingiliano, kubeba abiria na mizogo kupita kiasi na kushusha na kubeba abiria katika maeneo yasiyo rasmi.

Kamanda huyo alinukuu Biblia Zaburi 125:1 kifungu kisemacho, “Wamtegemeao Mungu ni kama mlima Zayuni, hawatatikiswa” akisema kampuni ya Narokline itafanikiwa kwa kumtanguliza Mungu.

Share This Article