Timu ya taifa ya Madagascar imeendeleza mazoezi kujiandaa kwa mechi ya robo fainali kuwania kombe la CHAN dhidi ya wenyeji Harambee Stars kesho kuanzia saa kumi na moja jioni katika uwanja wa kimataifa wa Kasarani.
Madagascar almaarufu Barrea,waliwasili nchini mapema wiki hii kutokea Dar es Salaam, Tanzania kujiandaa kwa mchuano huo muhimu huku wakilenga kufuzu kwa nusu fainali kwa mara ya pili mtawalia.
Barrea walimaliza katika nafasi ya pili kundini B kwa alama 7 wakishinda mechi mbili kutoka sare moja na kushindwa mara moja.
Upande wake Kenya waliomaliza wa kwanza kundini A wanashiriki CHAN kwa mara ya kwanza katika historia.
Robo fainali hiyo itakuwa ya kwanza na itafuatwa na ile baina ya Morocco dhidi ya wenyeji Tanzania.