Bunge la Taifa litarejelea vikao vyake leo Jumanne alasiri baada ya kumaliza mapumziko yake yaliyoanza mapema mwezi Disemba mwaka jana.
Bunge hilo linarejea vikao hivyo wakati ambapo Mahakama Kuu imetoa uamuzi ulioweka bayana kuwa muungano wa Azimio ndio ulio na wabunge wengi katika bunge hilo.
Viongozi wa Azimio, wakiongozwa na kinara wa Wiper Kalonzo Musyoka, wanashinikiza muungano huo kuchukua uongozi kama upande wa walio wengi katika bunge hilo kwa mujibu wa uamuzi wa mahakama.
Upande wa walio wengi kwa sasa unashikiliwa na muungano unaotawala wa Kenya Kwanza. baada ya Spika Moses Wetang’ula awali kutoa uamuzi ulioashiria kuwa muungano huo ndio ulio na wabunge wengi katika bunge hilo.
Wakati uamuzi huo ukiwa umebatilishwa na mahakama, macho ya wengi yataangazia kuona namna Wetang’ula atakavyoshughulikia suala hilo.
Isitoshe, Spika huyo alikuwa ameashiria kuwa kamati za bunge zitaundwa upya katika hatua ambayo huenda ikasababisha kutimuliwa kwa viongozi wa kamati mbalimbali wasiokuwa watiifu kwa utawala wa Kenya Kwanza.
Miongoni mwa wanaotazamiwa kuathirika katika mabadiliko hayo ni mbunge wa Kiharu Ndindi Nyoro ambaye ni mwenyekiti wa kamati ya bajeti.
Wakati wa kutimuliwa kwa Rigathi Gachagua kama Naibu Rais, mbunge huyo alionekana kutohusika mno isijulikane msimamo wake ulikuwa wapi.
Wabunge kutoka eneo la Kisii nao wamedai kutengwa katika uteuzi wa wabunge wa kuongoza kamati mbalimbali za bunge na kukinyoshea kidole cha lawama chama chao cha ODM.
Kuna jumla ya kamati 18 katika Bunge la Taifa.
Lingine litakaloangaziwa ni hatua itakayochukuliwa na Wetang’ula baada ya mahakama kutoa uamuzi kwamba hawezi akahudumu kama Spika wa Bunge la Taifa na pia kiongozi wa chama cha Ford K.