Rais William Ruto amewataka machifu na manaibu wao kuimarisha uongozi wao katika kuendeleza usalama na mageuzi ya kiuchumi ya Kenya, akisema maendeleo ya nchi yanategemea pakubwa kazi yao mashinani.
Akizungumza katika Chuo cha Mafunzo kwa Polisi cha Embakasi jijini Nairobi leo Disemba 1, 2025 Rais aliwasifia wasimamizi hao kwa kuwa kiungo muhimu kati ya serikali na wananchi, hasa nyakati za misukosuko.
Kiongozi wa nchi alibainisha kuwa ripoti ya Jukwaa la Usalama iliyozinduliwa hivi karibuni inaakisi kwa usahihi wasiwasi wa Wakenya kuhusu usalama na inatoa mapendekezo makhususi ya kuboresha utulivu wa umma na utoaji huduma.
Ruto alisema kwamba ingawa Kenya imeendelea kuwa thabiti kwa kiasi kikubwa, changamoto mpya kama migogoro ya kijamii, uhalifu unaochochewa na shinikizo za kiuchumi na majanga kama ukame zinahitaji uongozi wa kuchukua hatua mapema na uratibu wa karibu zaidi na wananchi.
Rais alisisitiza kuhusu programu muhimu za serikali chini ya ajenda ya mageuzi ya kiuchumi ya kuanzia chini kwenda juu, akitaja maendeleo makubwa katika kilimo, biashara ndogo na za kati, huduma za kidijitali, makazi na afya.
Alitaja usajili wa wakulima milioni 7.1 katika mpango wa mbolea ya ruzuku, upanuzi wa mifumo ya upatikanaji wa fedha kama Hustler Fund na NYOTA na kuwekwa kwa huduma zaidi ya 27,000 za serikali kwenye mfuj dijitali.
Ruto aliwahimiza wasimamizi kuhakikisha upatikanaji sawa wa huduma, kuhamasisha jamii kuhusu programu za serikali, na kupambana na upotoshaji wa taarifa, hasa kuhusu makazi na mageuzi ya kidijitali.
Akisisitiza umuhimu wao, Rais alisema ustawi wa Kenya “unategemea kwa kiasi kikubwa uongozi wenu katika ngazi za mashinani,” huku akiwataka machifu na manaibu wao kuendeleza juhudi za kudumisha utulivu, kuimarisha imani ya wananchi na kusukuma maendeleo ya taifa.
Machifu hao na manaibu wao walikuwa wanafuzu leo baada ya kukamilisha mafunzo.