Chama cha Mabaraza ya Vyombo vya Habari Duniani (WAPC) kimelaani vikali mauaji ya wanahabari wa runinga ya Al Jazeera katika Ukanda wa Gaza.
Al Jazeera imesema shambulizi la Israel katika ukanda huo lilisababisha vifo vya wanahabari wake watano.
Hii ni baada ya jeshi la Israel kushambulia hema wanamoishi wanahabari karibu na hospitali moja katika mji wa Gaza upande wa kaskazini juzi Jumapili.
Rais wa chama hicho David Omwoyo amelaani mauaji ya wanahabari hao wasiokuwa na hatia.
“Shambulizi hili lilifanywa kwenye hema la wanahabari karibu na hospitali ya al-Shifa katika mji wa Gaza City, shambulizi la wazi dhidi ya uhuru wa vyombo vya habari linalokusudia kuwanyamazisha wale wanaoripoti juu ya mgogoro wa Gaza,” alisema Omwoyo ambaye pia ni Mkurugenzi Mtendaji wa Baraza la Vyombo vya Habari nchini Kenya (MCK).
“Wanahabari hawa walikuwa waangalizi wasioegemea upande wowote, waliojitolea kuelezea ukweli na kupaza sauti za wanyonge. Hawakuwa wapiganaji, ilhali walilengwa kimakusudi, kwa madai yasiyokuwa na msingi yaliyotumiwa kutetea kuuawa kwao.”
Wanahabari wa Al Jazeera waliouawa ni Anas al-Sharif, Mohammed Qreiqeh, Ibrahim Zaher, Mohammed Noufal na Moamen Aliwa—na mwanahabari wa kujitegemea Mohammad al-Khaldi.
Kwenye taarifa, Mtandao wa Vyombo vya Habari wa Al Jazeera uliishutumu vikali Israel ukisema hili ni “shambulizi lingine la dhahiri na lililokusudiwa dhidi ya uhuru wa vyombo vya habari.”