Nigeria walianza kwa kishindo makala ya nane ya fainali za Kombe la Dunia kwa wasichana chini ya umri wa miaka 17 katika Jamhuri ya Dominica, baada ya kuichachafya Newzealand mabao 4-1 katika mechi ya kundi A jana usiku.
Katika pambano jingine kundini humo wenyeji Dominica walilabuliwa magoli mawili bila jibu na Ecuador, wakati Uhispania ikiwapiga laza Marekani magoli 2-1 katika kundi B.
Colombia na Korea Kusini waliambulia sare ya bao moja katika kundi B .

Kipute hicho kitaingia siku ya pili Alhamisi Oktoba 17, Japan wakimenyana na Poland katika kundi D saa tano usiku, huku Korea Kaskazini wakipimana ubabe na Mexico pia saa tano usiku katika kundi C.
Baadaye saa nane usiku Brazil watachuana na Zambia katika kundi D, wakati ambapo Kenya wakishuka uwanjani mida iyo hiyo dhidi ya Uingereza.