Spika wa bunge la kitaifa Moses Wetang’ula amekashfu baadhi ya viongzi wa kidini na mabalozi kwa kukosa kulaani ghasia, wizi na uharibifu wa mali ulioshuhudiwa wakati wa maandamanao ya Gen Z Jumatano.
Akizungumza wakati wa hafla ya utoaji uwezo kwa wanawake wa Lukuyani katika shule ya Matunda, Wetang’ula alitilia shaka kimya cha viongozi wa kidini na wanadiplomasia kuhusu uhalifu uliotanda siku ya maandamano.
“Kwanini viongozi wa dini na mabalozi wamekimya kuhusu ghasia, wizi na uharibifu wa mali na dhuluma za kimapenzi zilizotekelezwa na wahalifu wakati wa maandamanao ya Gen Z?” Wetang’ula aliuliza.
Spika huyo amesema inatia wasiwasi kwamba baadhi ya viongzi wa kidini na wanadiplomasia ambao wamekuwa wakiunga mkono wana Gen Z wamesalia kimya kuhusiana na uhalifu uliosheheni jijini Nairobi na maeneo mengine nchini.
“Ni jambo la kushangaza kwamba viongozi wa dini na mabalozi waliounga mkono maandamano hayo, sasa wamesalia kimya, hasaa baada ya maandamano hayo kugeuka na kuwa ghasia na kuhujumu mshikamano na usalama wa taifa,” aliongeza Spika huyo wa Bunge la Taifa.
Wetang’ula alitoa wito kwa viongozi wa kidini na wanadiplomasia kutokuwa na mapendeleo na kulaani uvunjaji sheria unapotokea pasina kujali makundi husika.
Kwenye tukio lisilo la kawaida spika huyo alionya aliyekuwa jaji mkuu David Maraga dhidi ya kuhusika kwenye maandamano ya kisiasa akisema uwepo wake kwenye maandamano ya Gen Z jijini Nairobi ni wakujutiwa.