Maandamano ya kizazi cha Gen Z yakitarajiwa kuandaliwa leo Jumatano, usalama umeimarishwa katikati ya jiji la Nairobi huku ukaguzi wa polisi ukitekelezwa.
Katikati ya Jiji la Nairobi ni mahame, biashara zikifungwa na magari ya uchukuzi wa umma katika baadhi ya barabara za jiji yamepunguza huduma zao, na kuwalazimu wasafiri kutafuta usafiri mbadala.
Maafisa wa polisi wameweka vizuizi vya usalama hususan katika maeneo ambayo yamelindwa kikatiba.
Barabara zinazoingia katikati ya Jiji la Nairobi zimefungwa, maafisa wa polisi wakishika doria. Barabara ya Ngong imefungwa katika mzunguko wa City Mortuary, huku ya Lang’ata ikifungiwa katika jumba la T-Mall. Barabara ya Jogoo imefungwa katika mzunguko wa Makongeni, ya Kiambu imefungwa katika klabu ya gofu ya Muthaiga huku barabara ya Valley imefungwa kuelekea Ikulu ya Nairobi.
Siku ya Jumanne, vijana na mashirika ya kijamii walifanya mkesha wa kuwasha mishumaa katika mtaa wa Tom Mboya jijini Nairobi kwa heshima ya wale waliopoteza maisha wakati wa maandamano ya mwaka jana.