Maandamano lazima yazingatie sheria, Mudavadi awaeleza mabalozi

Tom Mathinji
1 Min Read
Waziri Mwenye Mamlaka Makuu Musalia Mudavadi.

Waziri mwenye Mamlaka Makuu Musalia Mudavadi, ametetea serikali kuhusu jinsi ilivyoshughulikia maandamano yaliyoshuhudiwa hapa nchini Juni 25, 2025.

Mudavadi aliwafahamisha mabalozi wa kigeni kuwa, huku haki ya kuandamana ikilindwa na katiba, lazima maandamano yatekelezwe ndani ya sheria.

kupitia kwa taarifa kwa mabalozi hao iliyotolewa Alhamisi alasiri, Mudavadi alieleza kuwa maandamano yaliyokusudiwa kuwakumbuka waandamanaji waliofariki na kujeruhiwa mwaka 2024, yaligeuka na kuwa ghasia na uharibifu wa mali.

“Kutaja maandamano hayo kuwa halali, sio kuashiria uzalendo wa taifa hili,” alisema Mudavadi, akiongeza kuwa baadhi ya waandamanaji waliwashambulia wananchi, biashara, miundomsingi muhimu na taasisi za usalama.

Mudavadi aliyepia waziri wa Mambo ya Nje, alirejelea kuwa, kuandamana huambatana na uwajibikaji na kudumisha amani.

Aliwafahamisha mabalozi hao kuwa, ingawa haki ya kuandamana imekubaliwa na sehemu ya 33 ya katiba ya Kenya, haki hizo hazikubali kueneza propaganda, semi za chuki au uchochezi wa kikabila.

“Waandalizi wa maandamanao wanajukumu la kuhakikisha amani, huku ikiwa waandalizi wa maandamano haya hawajulikani na iwapo walitimiza hitaji lao la kikatiba,” aliongeza Mudavadi.

Aliwapongeza maafisa wa polisi kwa utaalam wao, akidokeza kuwa walizuia ghasia zaidi na kulinda amani ya kitaifa.

Share This Article