Waziri wa Usalama wa Taifa, Kipchumba Murkomen, amewaonya wanajeshi na maafisa wa polisi wa zamani dhidi ya kuhusika katika shughuli za uhalifu ambazo huenda zikaathiri taifa hili.
Akiongea leo Alhamisi mjini Nanyuki kwenye kaunti ya Laikipia wakati wa ziara ya usalama almaarufu Jukwaa La Usalama, waziri huyo alisema maafisa hao wa zamani sasa watachunguzwa kwa kina na serikali huku akihimiza idara ya mahakama kuhakikisha wale wanaohusika katika vitendo kama hivyo wanapewa hukumu ifaayo.
“maafisa wote wa polisi na jeshi ambao wameondoka kazini, wana wajibu muhimu kuwaliko wananchi. Tutawafuatilia kwa karibu, kwa sababu wamepokea mafunzo ya hali ya juu kutoka kwa serikali ya Kenya kuhusu utumizi wa silaha,” alisema Murkome.
Waziri Murkomen alisema maafisa wa zamani ambao wamebuni makundi yanayodaiwa kukabiliana na kile alichokitaja kuwa ukatili wa polisi wanafanya hivyo kwa manufaa ya kisiasa na kuleta dhana ili ionekana kana kwamba baadhi ya sehemu za taifa hili zinadhibitiwa na waasi.
Waziri Murkomen alishangaa ni kwa nini chama cha wanasheria nchini-LSK pamoja na mashirika mengine ya kijamii yanaweza kupinga mashtaka ya ugadi kwa watu kama hao.
Murkomen aliongeza kuwa serikali haitatishwa na itajitahidi vilivyo kulinda taifa hili bila ya kujali miegemeo ya kisiasa. Haya yanafuatia kukamatwa kwa afisa mmoja wa zamani wa KDF pamoja na maafisa wawili wa polisi wa zamani kwa kuvalia sare za kijeshi na kuonyesha silaha hadharani.