Waziri wa Usalama wa Taifa Kipchumba Murkomen, ametoa onyo kali kwa maafisa wa serikali wanaofanikisha utumizi wa mihadarati na pombe haramu katika kaunti ya Trans Nzoia na kwingineko, akisema chuma chao ki motoni.
Akizungumza Jumatatu katika kaunti ya Trans Nzoia, waziri huyo alielezea wasiwasi kuhusu ongezeko la utumizi wa pombe haramu kupitia usaidizi wa baadhi ya maafisa wa serikali, wakiwemo maafisa wa polisi, manaibu wa chifu na maafisa wa serikali ya taifa.
“Biashara inayoimarika hapa ya pombe haramu na mihadarati, ni kwa sababu baadhi ya maafisa wa serikali wale, wa usalama, wakiwemo maafisa wa polisi, wanashirikiana na wanabiashara hatari,” alisema Murkomen.
Ili kukabiliana na zimwi hilo, waziri huyo alitangaza kuwa Inspekta Jenerali wa Polisi atatuma kikosi maalum kutoka Makao Makuu ya Polisi, kufanya operesheni itakayowalenga walanguzi wa mihadarati kwenye kaunti ya Trans Nzoia.
Aidha, alidokeza kuwa maafisa wa usalama wafisadi, wataachishwa kazi na kushtakiwa, badala ya kuwahamisha.
“Tumekubali kwamba baadhi ya maafisa wetu ni wafisadi na tutakabiliana na wao mara moja na hatutahamisha afisa yeyote,” alisema Murkomen.
“Watapokea barua za kuachishwa kazi, huku wakiendelea na kesi zao mahakamani kujibu mashtaka kwanini wanafanikisha ulanguzi na usambazaji wa mihadarati na pombe haramu,” aliongeza waziri huyo.