Chama cha Maafisa wa Kliniki hapa nchini (KUCO), kimetoa ilani ya siku saba kabla ya kushiriki mgomo wa wanachama wake, unaotarajiwa kuanza Februari 18, 2025.
Maafisa hao walio chini ya mpango wa afya kwa wote (UHC), wametaja hatua ya serikali kukosa kushughulikia matakwa yao, yanayojumuisha masharti ya uajiri na usawazishaji wa mishahara miongoni mwa mengine.
Kupitia kwa taarifa leo Alhamisi, KUCO ilielezea kufadhaishwa kwake na kile ilichokitaja kuwa kutelekezwa na serikali na asasi zake, licha ya kuifahamisha serikali masaibu yake kupitia nyaraka kadhaa.
Masuala mengine ambayo chama hicho kinataka yaangaziwe ni pamoja na uwasilishaji wa matozo ya hazina ya kustaafu (NSSF) na marupurupu ya mishahara ya mwezi Mei mwaka 2024.
Aidha, chama hicho kinaishtumu serikali kwa kukiuka makubaliano ya kurejea kazini, yaliyotiwa saini Januari 14, 2025, kati ya Wizara ya Afya na Baraza la Magavana.
Chama hicho kililalamika kuwa licha ya kufutilia mbali mgomo uliopangwa awali kupitia barua iliyoandikwa Januari 17, 2025, makubaliano hayo bado hayajatekelezwa.