Kaimu Inspekta Jenerali wa polisi Gilbert Masengeli ametangaza kwamba kama wa kituo cha polisi cha Gigiri na maafisa 7 wa polisi wanaofanya kazi humo wamesimamishwa kazi kufuatia kutoroka kwa washikiwa 13.
Mshukiwa mkuu wa mauaji ya watu kadhaa ambao miili yao ilipatikana katika timbo la mawe eneo la Embakasi kaunti ya Nairobi Collins Jumaisi Khalusha na wengine 12 walitoroka kutoka kituo hicho cha polisi cha Gigiri.
Maafisa wa polisi walisema kwenye ripoti ya kisa hicho kwamba Jumaisi alihepa pamoja na raia 12 wa Eritrea waliokuwa wamekamatwa kwa kuwa nchini bila idhini.
Leo Jumanne Agosti 20, 2024 saa 11 asubuhi afisa wa polisi aliyekuwa kwenye zamu katika kituo cha polisi cha Gigiri kwa jina Gerald Mutuku, alizuru seli zote kama ilivyo ada akiwa na msimamizi wa duka la kituo hicho kuwapa washukiwa kiamsha kinywa.
Walipofungua seli walishangaa kupata kwamba hakukuwa na yeyote ndani kwani walihepa baada ya kukata nyaya za eneo ambao huwa wanaotea jua.
Jumaisi alikuwa ameshikiliwa katika kituo hicho cha polisi akisubiri kufikishwa mahakamani kukubali au kukataa mashtaka dhidi yake.
Maafisa wakuu wa idara mbali mbali za usalama walizuru kituo cha polisi cha Gigiri baada ya kupokea habari kuhusu kisa hicho akiwemo Inspekta Jenerali mteule Douglas Kanja na mkurugenzi wa idara ya upelelezi wa jinai DCI Mohamed Amin.