Maafisa wa DCI wawakamata washukiwa wawili wa ujambazi Nairobi

Tom Mathinji
2 Min Read
Washukiwa wa ujambazi wakamatwa Nairobi.

Maafisa wa upelelezi wa makosa ya jinai DCI, wamewakamata washukiwa wawili wanaodaiwa kuhusika katika wizi uliotekelezwa kwenye duka moja la jumla, ambapo bidhaa zenye thamani ya takriban shilingi milioni 17.6 ziliibwa.

Kulingana na DCI, washukiwa hao wanadaiwa walivamia kituo cha kibiashara cha Atlantic Business katika mtaa wa Embakasi mnamo Aprili 20,2025, na kupora mali iliyomilikiwa na kampuni ya Aetlantiq Group Limited.

Kupitia mtandao wake wa X, idara hiyo ilisema wafanyakazi wa kampuni hiyo waliwasili kazini baada ya Siku Kuu ya pasaka na kupata bidhaa zimeibwa, baada ya majambazi kuingia ndani ya jengo hilo kupitia paa.

Walinzi wa jengo hilo ambao walitoweka, walikosa kuwafahamisha maafisa wa husika wakati king’ora cha jengo hilo kilipolia, na kuzua tashwishi kuhusu kuhusika kwao katika wizi huo.

Maafisa wa polisi walianzisha uchunguzi na kuwakamata James Macharia Mwangi na mshirika wake Keriko Wanjama, baada ya kupatikana katika maficho yao kwenye hoteli moja mtaani Ruai.

Washukiwa hao walipatikana na baadhi ya bidhaa zinazoshukiwa kuwa sehemu ya zile zilizoibwa. Bidhaa hizo zinajumuisha Televisheni kadhaa na vifaa vingine vya elekroniki.

Maafisa hao pia walipata lori aina ya Mitsubishi yenye nambari za usajili KAV 565Q, lililokuwa na bidhaa ndani yake.

Bidhaa hizo na lori hilo zinazuiliwa na maafisa wa polisi huku uchunguzi zaidi ukiendelea.

Share This Article