Tarehe 3 Septemba mwaka huu mjini Beijing China, kulikuwa na shughuli kubwa ya maadhimisho ya miaka 80 ya ushindi wa mapambano ya watu wa China dhidi ya uvamizi wa Japani, na ushindi wa vita ya dunia dhidi ya ufashisti. Viongozi wakubwa kutoka nchi mbalimbali duniani, walishiriki kwenye maadhimisho hayo, na kuangalia gwaride kubwa la maadhimisho ya ushindi huo.
Ni miaka 80 sasa imepita tangu China na dunia ziwe kwenye mateso makubwa ya ufashisti duniani, na sasa kwa ujumla dunia iko kwenye mwelekeo tofauti kabisa, ambao unazingatia kuheshimu utu, uhai na hata heshima ya binadamu.
Bahati mbaya kutokana na historia na mfumo wa elimu wa Tanzania, watanzania wengi tunahusisha ufashisti na ukatili uliofanywa na utawala wa Adolf Hitler wa Ujerumani, na ule wa Benito Mussolini wa Italia, dhidi ya watu waliotofautiana nao kiitikadi, kwa asili au hata nia tu ya kutaka kutawala. Ukweli ni kwamba barani Asia, na hasa nchini China ufashisti ulionekana kwa sura ya kikatili ambayo haielezeki, na ni bahati mbaya tu kuwa vyombo vya habari vya magharibi na mfumo wa elimu wa kimagharibi, uliweka mkazo kwenye medani ya Ulaya, na kudogosha ukubwa wa ukatili uliofanyika nchini China.
Lakini kutokana na umahiri wa wachina kutunza na kuthamini kumbukumbu za historia kupitia njia mbalimbali, ikiwemo sekta ya filamu, watu wa nchi mbalimbali duniani sasa wanajua ni nini kilitokea nchini China. Kwa mfano, filamu mpya ya China kuhusu mauaji ya kimbari ya Nanjing ya mwaka 1937 iitwayo “Dead to Rights”, ambayo kwa mara ya kwanza imeoneshwa mjini Dar es Salaam, imewashitusha watu wengi walioitazama hasa kutokana na ukatili usioelezeka uliofanywa na wanajeshi wa Japani. Ni ukatili wa kutisha dhidi ya watu ambao hawakuwa na uwezo wowote wa kupigana au hata kujitetea waliokimbilia kwenye studio moja ya kupiga picha kutafuta hifadhi.
Ukatili ulioonyeshwa kwenye filamu hiyo ya China, ni sehemu ndogo tu ya ukatili ambao ushahidi wake umehifadhiwa, lakini kuna matendo mengi tu ya kikatili yasiyo na ushahidi wa maandishi au picha, ambayo hadi leo ni donda ndugu miongoni mwa wachina na watu wengine wa Asia.

Wiki hii kilichoonekana mjini Beijing ni cha kuvutia, yaani gwaride kubwa la kijeshi, na zana mbalimbali za kivita zilizooneshwa katika uwanja wa Tian’anmen mjini Beijing, na kuhudhuriwa na viongozi na wakuu wa nchi 26 kutoka sehemu mbalimbali duniani. Kuhudhiriwa na idadi kubwa ya viongozi kutoka nje, kunaonyesha kuwa sehemu kubwa ya dunia inatambua madhara yaliyoletwa na ufashisti duniani haswa katika medani ya China, lakini pia ni kuonyesha dunia kuwa kuna mambo muhimu tunayotakiwa kukumbuka.
Kwanza, tunaishi katika dunia ambayo baadhi ya wanasiasa na wanataaluma wenye hila, wameanza kujaribu kuficha madhambi yaliyofanywa na wafashisti duniani. Kuna baadhi wanajaribu kuleta machapisho yenye marekebisho ya historia au kupotosha historia, ili kupuuza kiini cha uchokozi wa wafashisti, au hata kutetea baadhi ya vitendo vilivyofanywa na wafashisti. Wengine wanajaribu kudogosha mchango wa China katika ushindi mpana wa washirika kwenye mapambano dhidi ya ufashisti kwenye medani ya Asia. Na kuna wengine kwa makusudi kabisa, wanachanganya sababu ya kupambana na ufashisti na siasa za vita baridi, na hivyo kujaribu kufuta mshikamano wa kweli wa binadamu wa zama ile ya mapambano dhidi ya ufashisti.
Pili, dunia imeanza kushuhudia mwelekeo ambao haukufikirika miaka 10 iliyopita. Dunia imeanza kuona wanasiasa na siasa za itikadi kali, na kuibuka kwa makundi ya wafuasi wa siasa hizo ambao hawana hata haya ya kujificha tena. Baadhi ya wanasiasa duniani wamekuwa na ujasiri wa wazi kabisa wa kuiga au hata kufanya vitendo ambavyo vinalingana kabisa na siasa za itikadi kali. Katika baadhi ya nchi duniani kuna vyama vyenye mrengo wa kifashisti ambavyo vinafanya kampeni wazi za kueneza chuki, na vingine vimekuwa hata sehemu ya serikali.
Ni kutokana na sababu hizo, kuadhimisha ushindi wa mapambano ya wachina dhidi ya uvamizi wa Japani, na ushindi wa vita ya dunia dhidi ya ufashisti, sio tu ni kitendo cha kukumbuka yaliyopita, bali ni kuitahadharisha dunia kuhusu uwezekano wa kurudi kwa janga hilo kama dunia haitakuwa macho.
Wakati ufashisti ulipotamalaki barani Ulaya, kilikuwa ni kipindi ambacho nchi za Ulaya zilikuwa zinapata maendeleo makubwa ya kiuchumi, na ilionekana kuwa ufashisti ni moja ya njia za kulinda maendeleo ya nchi zenye nguvu kwa wakati ule. Japani nayo ilikuwa ni nchi iliyotangulia kupiga hatua za maendeleo ya kiuchumi na kijeshi kuliko majirani zake, ilitumia kisingizio kama hicho cha nchi za Ulaya kuvamia nchi nyingine na kufanya ukatili.
Tofauti na nchi hizo, China inajipatia maendeleo yake kwa amani na kuchangia maendeleo ya kimataifa kupitia mipango yake mbalimbali kama vile “Ukanda Mmoja, Njia moja” BRI na mapendekezo mbalimbali. Mipango hiyo sio tu inahimiza maendeleo ya uchumi, bali pia kuhimiza amani duniani.
