Lupita Nyong’o na kakake kuigiza pamoja

Wataigiza 'Twelfth Night' igizo la vichekesho lililoandikwa na William Shakespeare.

Marion Bosire
2 Min Read

Mwigizaji Lupita Nyong’o na kaka yake Junior Nyong’o wataigiza pamoja kama mapacha katika igizo la vichekesho la Shakespeare liitwalo ‘Twelfth Night’.

Lupita ambaye amewahi kushinda tuzo ya Oscar alifichua hayo kupitia mitandao ya kijamii ambapo alichapisha picha ya pamoja na kakake Junior Nyong’o na kudhihirisha msisimuko wa kipekee.

“Ninafurahia kufichua maajabu fulani ya kutizamia, kakangu Junior Nyong’o na mimi tutaingia jukwaani kama mapacha.” aliandika binti huyo wa Gavana wa Kisumu Anyang Nyong’o.

Aliendelea kuelezea kuhusu igizo hilo ambapo wataigiza kama Viola na Sebastian. “Naweza kusema tu kwa uhalisia kwamba tumekuwa tukijitayarisha kwa majukumu haya maisha yetu yote.” aliandika Lupita.

Igizo lao la jukwaani litakuwa katika ukumbi wa maonyesho ya sanaa uliokarabatiwa wa Delacorte huko Central Park Agosti 7 hadi Septemba 14, 2025.

Mwelekezi wa igizo hilo ni Saheem Ali na uzinduzi rasmi utafanyika Agosti 21, 2025.

Waigizaji wengine waliohusishwa ni Peter Dinklage atakayeigiza kama Malvolio, Jesse Tyler Ferguson atakayeigiza kama Andrew Aguecheek na Sandra Oh ambaye ataigiza kama Olivia kati ya wengine wengi.

Twelfth Night ni mojawapo ya maigizo yanayopendwa sana ya vichekesho yaliyoandikwa na Shakespeare. Linasimulia hadithi ya mapacha Viola na Sebastian.

Wawili hao wanatenganishwa na kuzama kwa meli na Viola analazimika kujisingizia kuwa mwanaume kwa usalama wake.

Hata hivyo anajipata katika mvutano wa kimapenzi ambapo amempenda Duke Orsino, lakini Duke anampenda Olivia ambaye naye amevutiwa na Viola asijue ni mwanamke kama yeye.

Hii ni mara ya saba igizo hilo la Twelfth Night linafanyika katika ukumbi wa Delacorte.

Liliwahi kuandaliwa humo miaka ya 1969, 1986, 1989, 2002, 2009 na 2018.

Share This Article