Chama cha wanasheria nchini LSK kimetoa wito kwa mamlaka za serikali kuchukua hatua za dharura na kuharakisha uchunguzi wa mauaji ya wengi yanayodaiwa kutekelezwa na maafisa wa polisi wakati wa maandamano ya Gen Z mwaka jana.
Katika taarifa kwenye mkutano na wanahabari, maafisa wa LSK walilaani vikali mauaji ya kiholela ya wakenya wasio na silaha na wakatahadharisha kuwa ukiukaji unaoendelea wa haki ya kuishi ni tishio kubwa kwa demokrasia ya Kenya, mamlaka ya kitaifa na utawala wa kikatiba.
Wakirejelea haki ya kuishi kama ilivyo kwenye Ibara ya 26 ya Katiba, mawakili hao walielezea hali ya sasa kama kejeli ya kusikitisha ambapo vyombo vya usalama vya serikali vilivyojukumiwa kulinda raia sasa vimegeukia ukatili.
Hali hii ilijitokeza wazi baada ya makala ya uchunguzi ya BBC Africa Eye ya Aprili 27, 2025, ambayo yalishtua taifa kwa kufichua mauaji ya kutisha yaliyotekelezwa na maafisa dhidi ya waandamanaji vijana.
Siku moja baadaye, watu wengine sita waliuawa katika eneo la Angata Barrikoi huko Kilgoris, kaunti ya Narok, wakati wa maandamano ya amani na hivyo kuongeza hasira miongoni mwa umma.
LSK ilitaja mauaji hayo kuwa uhalifu wa wazi na kuitaka serikali kuwachukulia hatua za kisheria wahusika mara moja.
LSK pia ilieleza wasiwasi mkubwa juu ya matamshi ya dharau kutoka kwa viongozi wa kisiasa, wakiwemo Wabunge Bashir Abdullahi, Peter Kaluma, na John Kiarie, waliopuuza mauaji hayo na kuhoji uhalali wa ripoti ya BBC.
LSK ilisema kauli hizo zinapuuza ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu na kudhalilisha heshima ya majukumu ya Bunge.
Ikiwaonya viongozi kuhusu kuvunjika kwa imani ya umma na kuyumba kwa uthabiti wa kitaifa, LSK ilizitaka mamlaka zinazohusika — ikiwemo Mamlaka Huru ya Kusimamia Polisi (IPOA), Tume ya Huduma ya Polisi na Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma — kuchukulia uchunguzi huu kwa uzito wa hali ya juu.
Kati ya kesi 60 za unyanyasaji wa polisi zilizowasilishwa kwa IPOA, ni sita pekee ndizo zilizokamilika na kupelekwa kwa hatua zaidi — kasi ambayo LSK ilisema ni dalili ya “kutowajibika kwa dhahiri.”
LSK ilihimiza wadau wote, wakiwemo Bunge na Baraza la Usalama la Kitaifa, kuunga mkono uchunguzi kamili wa mauaji ya kiholela — ya sasa na ya kihistoria — ili kuhakikisha haki kwa waathiriwa na uwajibikaji kwa wahusika.
“Wakati wa kulegeza kamba umeisha,” taarifa hiyo ilisema. “Kushindwa kuchukua hatua kutazidisha mzozo, kuhatarisha utawala wa kikatiba, na kusaliti imani ya wananchi wa Kenya.”