Mwanamuziki wa Uganda Yasin Mukasa maarufu kama Lil Pazo amewajibu wanaokosoa muziki wake wakiutaja kuwa wa muda mfupi, unaotegemea mitindo na wakati mwingine una maneno machafu.
Pazo anasisitiza kwamba nyimbo zake zitasalia muhimu kwa mashabiki kwa muda mrefu kiasi kwamba hata watoto wake watazisikiliza na kuzipenda.
Alifananisha safari yake ya muziki na ile ya bendi maarifu ya Afrigo ambayo imesalia kuwa muhimu na kupendwa na wengi kwa miongo kadhaa, kuanzia wakati wa uongozi wa Iddi Amin.
Msanii huyo anasema kwamba wale mashabiki ambao walikuwa wakisikiliza kazi za bendi ya Afrigo wakiwa vijana ndio bado wanafurika kwenye matamasha yao hadi sasa.
Haya yanajiri siku chache tu baada ya msanii na mwanasiasa Bobi Wine kushauri wasanii wa kizazi kipya kuwa makini na maneno wanayotumia kwenye muziki.
Alisema kwamba wanajiweka katika hatari ya kusahaulika haraka.