Kenya itamenyana na Cameroon leo kuanzia saa moja usiku katika uwanja wa Ahmadou Ahidjo Japoma mjini Yaounde, Cameroon katika mechi ya kundi J kufuzu kwa kipute cha AFCON mwaka ujao.
Harambee Stars waliwasili Douala jana Alhamisi tayari kwa pambano hilo, wakipigwa jeki na kurejea kwa mshambulizi na nahodha Michael Olunga aliyekosa mechi mbili za mwezi jana.
Timu hizo zinakutana kwa mara ya tano leo katika mechi za kimataifa huku Cameroon – Indomitable Lions, wakiibuka kidedea mara tatu na mchuano mmoja kuishia sare tasa.

Harambee Stars walishindwa na Indomitable Lions mabao 2-1 Februari 23, 1972 katika mechi ya AFCON wakati wa mashindano yaliyoandaliwa mjini Douala.
Mechi ya pili kati ya Kenya na Cameroon ilikuwa hatua ya makundi ya kipute cha AFCON Machi 20, 1988 nchini Morocco iliyoishia sare tasa.
Harambee Stars walikutana kwa mara ya tatu na Simba wasiotikisika wa Cameroon tarehe 9 mwezi Machi mwaka 1990 katika mechi ya makundi ya AFCON nchini Algeria ambapo Cameroon walisajili ushindi wa 2-0.

Mara ya mwisho kwa Kenya na Cameroon kuchuana ilikuwa katika mechi ya kimataifa ya kirafiki Januari 9 mwaka 2010 katika uwanja wa kimataifa wa Kasarani, Indomitable Lions wakiinyuka Kenya mabao 3-1.
Cameroon waliishinda Namibia bao moja kwa nunge katika mechi ya kwanza mjini Yaounde, kabla ya kutoka sare tasa dhidi ya Zimbabawe mjini Harare.
Harambee Stars walianza kwa sare tasa dhidi ya Zimbabwe jijini Kampala katika mechi ya kwanza ya kundi J, kabla ya kuwalemea Namibia 2-1 mwezi jana katika mechi iliyochezewa mjini Johannesburg.

Zimbabwe walioishinda Namibia goli 1 kwa bila jana, wanaongoza kundi J kwa pointi 5, wakifuatwa na Kenya kwa alama 4 sawia na Cameroon, huku Brave Warriors ya Namibia ikishika nanga bila alama.
Kenya itawaandaa Cameroon Jumatatu ijayo, Oktoba 14 kuanzia saa kumi jioni katika uwanja wa Nelson Mandela jijini Kampala, Uganda kwa mechi ya marudio.
Mechi ya leo kati ya Cameroon na Kenya itaanza saa moja kamili usiku majira ya Afrika Mashariki na kupeperushwa mubashara kupitia runinga ya taifa ya KBC Channel 1.