Ukraine na Urusi wameendelea kushutumiana kwa kukiuka mpango wa kusitisha mapigano kwa ajili ya Pasaka uliotangazwa na Rais wa Urusi, Vladimir Putin, ambao Ukraine ilisema ulianza kukiukwa mara tu baada ya kutangazwa.
Katika kipindi kifupi cha utulivu kinachokaribia kuisha, Rais wa Ukraine Volodymyr Zelenskyy alitoa taarifa kupitia kwa Kamanda wa Jeshi Oleksandr Syrskii, akibainisha kwamba kuanzia mwanzo wa siku jeshi la Urusi limevunja amri ya kusitisha mapigano ya Putin zaidi ya mara elfu mbili.
Hata hivyo, kiongozi huyo wa Ukraine alisema hakujakuwa na milio ya mizinga au mashambulizi ya makombora siku ya Jumapili, na alipendekeza kuwa Moscow iacha mashambulizi ya ndege zisizo na rubani na makombora dhidi ya miundombinu ya kiraia kwa angalau siku 30.
Msemaji wa ikulu ya Urusi almaarufu Kremlin, Dmitry Peskov, alinukuliwa akisema kuwa Putin hatorefusha mpango huo wa kusitisha mapigano.
Mpango huo ulitarajiwa kufikia kikomo usiku wa manane Jumapili huku wizara ya masuala ya kigeni ya Marekani ikisema ingependelea muda huo uongezwe.
Katika tangazo la kushtukiza siku ya Jumamosi, Putin aliamuru majeshi yake kusitisha shughuli zote za kijeshi za mstari wa mbele wa vita dhidi ya Ukraine, akitaja sababu za kibinadamu.
Usitishaji huo wa mapigano wa saa 30 ungedhihirisha hatua kubwa zaidi ya utulivu katika vita vilivyodumu zaidi ya miaka mitatu.
Lakini saa chache tu baada ya amri hiyo kuanza kutekelezwa Jumamosi, tahadhari za mashambulizi ya anga zilisikika Kyiv na katika maeneo mengine ya Ukraine, huku Zelenskyy akiishutumu Urusi kwa kuendelea na mashambulizi yake na kuonyesha kuwa ilikuwa ni mbinu ya kupambana na upinzani wa kimataifa kwa propaganda.
Wizara ya Ulinzi ya Urusi pia ilidai siku ya Jumapili kuwa Ukraine ilikiuka mpango huo wa kusitisha mapigano zaidi ya mara 1,000.