Julius Kyazze mmoja wa waanzilishi wa kampuni ya muziki inayosimamia pia wasanii, Swangz Avenue amethibitisha kwamba mwanamuziki Winnie Nwagi bado ni msajiliwa wa kampuni hiyo.
Kyazze alisema hayo katika mahojiano kwenye runinga ya NBS Februari 24, 2025 ambapo alifafanua kwamba wanashirikiana na mwanamuziki huyo kwa namna tofauti.
“Tunafanya kazi na Winnie kwa njia tofauti. Tunahusika na usambazaji wa muziki wake. Tunashughulikia maombi ya wateja wake. Tunasimamia kazi zake za utangazaji wa bidhaa na huduma za kampuni nyingine.” Alisema Kyazze.
Kyazze alielezea kwamba mikataba ya wasanii hubadilika kila mara na iwapo kutakuwa na utofauti katika mkataba wa Winnie basi wataweka wazi mabadiliko hayo.
Usemi wake unafuatia uvumi ambao umeibuka tena kwamba Winnie Nwagi na meneja wake George Bakuuta Gonzaga wameondoka Swangz Avenue.
Kampuni ya Swangz Avenue alisema inabadilika pia na kuwa bora zaidi inapoingilia masoko mapya na kwamba hivi karibuni itatangaza usajili wa msanii kutoka nchini Tanzania.
Mapema mwezi huu, Winnie Nwagi mwenyewe alilazimika kuzungumzia uvumi kwamba ameondoka kwenye kampuni hiyo.
Alitia saini mkataba wa miaka mitano na Swangz mwaka 2020 na ulifikia kikomo hivi maajuzi na ripoti zikaibuka kwamba alikuwa akijikokota kutia saini kataba mwingine.
Wakati akitumbuiza katika eneo la burudani la Villa huko Bukoto, mashabiki zake walitaka kufahamu ukweli kuhusu suala hilo ambapo alisema kwamba bado yuko chini ya usimamizi wa Swangz huku mambo yakitatuliwa.
Alikanusha pia madai kwamba alikuwa ameelekeza maejenti wake wa kumtafutia kazi za utumbuizaji wasizipitishie Swangz Avenue.
Iwapo ametia saini mkataba mwingine na Swangz Avenue basi atakuwa msanii ambaye amedumu muda mrefu zaidi kwenye kampuni hiyo aliyojiunga nayo mwaka 2014.