Serikali ya Kaunti ya Kwale imezindua rasmi zoezi la ukusanyaji wa maoni ya wananchi kuhusu Bajeti ya Ziada ya Mwaka wa Kifedha 2024/2025, Mswada wa Kifedha wa mwaka 2025/2026, pamoja na Sheria ya Utekelezaji wa Hazina ya Biashara ya Wadi katika maeneo ya Tiwi, Ng’ombeni, Bongwe-Gombato, Ukunda na Kinondo.
Zoezi hilo litafanyika kwa siku nne na linalenga kufikia wananchi katika wadi zote 20 za Kaunti ya Kwale.
Kaunti ya Kwale imejizolea sifa kitaifa baada ya kuorodheshwa na shirika la kimataifa la International Budget Partnership (IBP) kuwa nambari moja nchini kwa kuhusisha wananchi kikamilifu katika mchakato wa bajeti na utekelezaji wa miradi ya maendeleo.
Kwa mujibu wa Mwenyekiti wa Jopo la Bajeti la Kaunti, Patrick Yasisi, mchakato wa ukusanyaji maoni una umuhimu mkubwa katika kusaidia serikali ya kaunti kupanga na kutekeleza miradi inayotokana na maoni na mahitaji ya wananchi.
“Kupitia maoni haya, serikali inaweza kupanga maendeleo kwa ushirikiano na jamii, hivyo kuepuka migogoro na kuhakikisha miradi inakidhi matarajio ya wananchi,” alisema Yasisi.
Zoezi hili linatarajiwa kukamilika siku ya Alhamisi, tarehe 22 Mei 2025, kabla ya kuwasilishwa kwa Bunge la Kaunti ya Kwale kwa ajili ya kujadiliwa na kuidhinishwa rasmi.