Kutoka kitunguu kibichi hadi fursa: Jinsi vitunguu vinavyobadilisha maisha Nyandarua

Martin Mwanje
3 Min Read

Kaunti ya Nyandarua, inayojulikana kwa udongo wake wenye rutuba na hali ya hewa ya baridi, imekuwa kitovu cha kilimo cha mazao muhimu kama vile mbaazi, karoti, kabichi, na vitunguu. Mazao hayo hayalishi tu jamii za kaunti hiyo bali pia husambazwa katika masoko ya Kenya nzima na hata nchi za nje.

Hivi majuzi, wakulima katika maeneo kama Kipipiri wameanza kuhama kutoka kwa mazao ya kawaida hadi kwa fursa zenye faida zaidi kama vile vitunguu.

Mmoja wa wakulima hao ni Esther Muthoni Njogu kutoka kijiji cha Mwangaza, Kipipiri, ambaye ameanza kulima aina hii ya vitunguu yenye mavuno ya haraka na faida kubwa.

Tulimpata Esther akihudumia shamba lake la vitunguu vibichi, ambapo alieleza kuwa zao hilo ni rahisi kutunza na huleta kipato kizuri.

“Kwa kipande kidogo tu cha ardhi, naweza kuvuna mara tatu au nne kwa mwaka,” alisema.

“Hii imenisaidia kusomesha watoto wangu na kutunza familia yangu kwa urahisi.”


Mradi wa Muthoni pia umeleta ajira katika kijiji chake, kuanzia maandalizi ya shamba hadi palizi na uvunaji. Vijana na wanawake wa eneo hilo wananufaika na kazi za mkono ambazo sasa zimekuwa za mara kwa mara kutokana na mzunguko mfupi wa miezi mitatu wa zao hilo.

Kwa upande wake, Newton Ng’ang’a, mkulima mwingine wa vitunguu kutoka kijiji cha Turasha, Kipipiri, anathibitisha faida za mazao ya mzunguko mfupi. “Mazao ya miezi mitatu ni mazuri kwa sababu huleta kazi kijijini,” anasema.

“Nawahimiza vijana waombe wazazi wao hata robo au nusu ekari walime vitunguu, beetroot, au dania badala ya kupoteza muda katika vituo vya biashara wakinywa pombe zilizochanganywa.”

Ng’ang’a pia anazungumzia suala la matumizi ya dawa za kuua wadudu.

“Tunahakikisha tunatumia kiasi kidogo cha kemikali hatari,” anaeleza.

“Ukipulizia dawa ya baridi mara moja, mara nyingi inatosha kwa msimu. Zaidi ya hayo, tunapendelea kutumia mbolea ya asili.”

Zaidi ya kilimo, Esther Njogu ana ujumbe kwa viongozi wa eneo. Anawaomba Wabunge kutoka Kaunti ya Nyandarua kusimamia sera zinazowalinda wakulima wa ndani.

“Wanapaswa kuwasilisha mswada bungeni kuzuia uagizaji wa chakula bila ushuru ambacho kimejaa masoko yetu,” anasema. “Mazao yetu ya hapa ni salama, safi, na yanaendeleza maisha ya wananchi.”

Mbali na vitunguu, Esther pia hulima dania na mboga zingine, na kugeuza shamba lake kuwa chanzo cha chakula na kipato cha kudumu.

Kauli zao za mwisho ni fupi lakini zenye uzito: “Kilimo kinawalipa. Ukiwa na zao sahihi na bidii, hata kipande kidogo cha ardhi kinaweza kubadilisha maisha yako.”

Share This Article