Kuna njama ya kuniondoa afisini, asema Gavana Wamatangi

Tom Mathinji
1 Min Read
Gavana wa Kiambu Kimani Wamatangi akiwahutubiwa wakazi wa Ngoliba, kaunti ndogo ya Thika Mashariki, kaunti ya Kiambu.

Gavana wa Kiambu Kimani Wamatangi, amesema mitego imewekwa katika pembe zote za kaunti hiyo kwa lengo la kumuondoa afisini.

Wamatangi ambaye hivi juzi alikamatwa na maafisa Maadili na Kukabiliana na Ufisadi EACC kuhusu madai ya ufisadi, alisema makundi ya watu wafisadi na baadhi ya wanasiasa wanapanga njama za kumuondoa mamlakani.

Akizungumza katika soko la Ngoliba, kaunti ndogo ya Thika Mashariki wakati wa zoezi ya kusambaza mbolea bila malipo kwa wakulima, Gavana huyo alishikilia kuwa hatayumbishwa na atatekeleza ahadi zake kwa wakazi wa kaunti hiyo.

“Mitego mingi imewekwa katika pembe zote za kaunt. Wanasiasa na makundi ya wafisadi wanataka niondoke kutokana na msimamo wangu mkali kuhusu ufisadi na uporaji wa mali ya umma,” alisema Gavana huyo.

Alidokeza kuwa watu wafisadi wamekuwa wakimezea mate vipande vya ardhi katika kaunti hiyo, huku akisimama kidete kulinda ardhi hiyo dhidi ya unyakuzi.

Aidha, alisema tangu alipochukua hatamu za uongozi, mapato ya kaunti hiyo yameongezeka maradufu kutoka shilingi bilioni 2.9 mwaka 2022 hadi shilingi bilioni 4.7 mwaka 2025.

Share This Article