Kukatika kwa umeme kwatatiza biashara mji wa Murungaru, eneo la Kinangop

Martin Mwanje
1 Min Read

Biashara katika mji wa Murungaru, ulioko eneo la Kinangop katika Kaunti ya Nyandarua, zimeathirika pakubwa baada ya kukatika kwa umeme kwa muda wa siku tatu mfululizo.

Transfoma inayosambaza umeme katika eneo hilo iliharibika, na licha ya mafundi kutoka kampuni ya Kenya Power kufika kukagua, tatizo hilo halijatatuliwa hadi kufikia siku ya tatu.

Hali iliyowaacha wakazi wengi na wamiliki wa biashara bila umeme.

Katika mji wa Ndunyu Njeru, baadhi ya wafanyabiashara waliandaa maandamano ya amani wakitaka transfoma hiyo ibadilishwe haraka, wakieleza kuwa kukosekana kwa umeme kumetatiza shughuli zao za kila siku na kusababisha hasara kubwa.

Wafanyabiashara waliathirika kwa kulazimika kufunga maduka yao mapema au kutofungua kabisa kutokana na ukosefu wa umeme.

Wamelalamikia pia juhudi zao za kuwasiliana na maafisa wa Kenya Power kupitia simu na njia zingine ambazo hazijazaa matunda, kwani hawajapokea msaada wowote wala majibu ya kuridhisha.

Jitihada zetu za kumpata afisa wa Kenya Power anayesimamia eneo hilo hazikufua dafu kufikia wakati wa kuchapishwa kwa taarifa hii.

 

Share This Article