Kukamatwa kwa VeryDarkMan kwazua tumbo joto Nigeria

Mkosoaji huyo alikamatwa nje ya benki ya GTB jijini Abuja alikokuwa amekwenda kulalamikia utoaji kiholela wa hela kutoka kwa akaunti ya mamake.

Marion Bosire
2 Min Read
VDM

Mkosoaji maarufu wa Nigeria ambaye pia ana ushawishi mkubwa mitandaoni Martins Vincent Otse maarufu kama VeryDarkMan -VDM alikamatwa na maafisa wa polisi hali ambayo imezua wasiwasi kati ya mashabiki wake.

VDM alikamatwa alipokwenda kwa benki ya GTB mjini Abuja kuwasilisha malalamishi baada ya pesa kuondolewa mara kwa mara kwenye akaunti ya mamake mzazi bila idhini.

Kulingana na wakili wa VDM aitwaye Deji Adeyanju, mkosoaji huyo alikamatwa na maafisa wa kitengo cha tume ya kukabiliana na uhalifu wa kiuchumi na kifedha EFCC ambao hawatoa maelezo kamili ya kumkamata.

Sasa wanamitandao wa Nigeria wanataka aachiliwe mara moja wakisema alikuwa amekwenda kuwasilisha malalamishi yake hatua ambayo ni haki yake.

Mhubiri maarufu nchini Nigeria Primate Ayodele alilalamikia kukamatwa kwa VDM akisema kila raia wa Nigeria ana haki ya kupaaza sauti na kutoa maoni.

Huku akitaka kwamba VDM aachiliwe mara moja bila masharti, Ayodele alisema kwamba kunyamazisha watetezi kwa kuwakamata kuna madhara makubwa kwa maadili ya demokrasia.

Mwanamuziki Portable naye ameomba maafisa wa EFCC pamoja na usimamizi wa benki ya GTB wamwachilie huru VDM ambaye anamrejelea kama rafiki yake.

Kwenye video aliyochapisha katika mtandao wa X, Portable alielezea kwamba hata ingawa huwa wanavutana na VDM mara kwa mara, anampenda na anapenda anavyosaidia watu.

“Jamani, kwa ajili ya Mungu. Naomba mmwachilie VeryDarkMan, yeye ni rafiki yangu. Huwa anagawa chakula kwa watu, yeye husaidia watu wengi. Ninapenda watu ambao husaidia wengine.” alisema Portable.

Mwanamuziki maarufu Davido naye hajaachwa nyuma katika kutafuta uhuru wa VDM. Alitumia akaunti yake ya mtandao wa X ambapo alimsifia VDM kwa kugusa maisha ya raia wengi wa Nigeria akitaka aachiliwe huru.

Wanasiasa na watu wengine wenye ushawishi mkubwa nchini Nigeria wamepaaza sauti zao wakitaka mkosoaji huyo aliyekamatwa Ijumaa aachiliwe huru.

Share This Article