Katika moyo wa mji wa Nyahururu, tukio la kipekee lilifanyika wakati wa Mkutano wa Kiuchumi na Uwekezaji wa kaunti ya Laikipia, likiwakutanisha viongozi, wajasiriamali, wawekezaji na washirika wa maendeleo. Mkutano huo uliweka Laikipia katika ramani kama kielelezo cha ukuaji, ubunifu, na fursa — hasa kwa vijana na wafanyabiashara wadogo wanaotafuta kushiriki katika juhudi za kuufufua uchumi wa Kenya.
Mwenyekiti wa Bodi ya Mamlaka ya Mapato humu nchini (KRA), Ndiritu Muriithi, alisisitiza kuhusu ongezeko la Pato Ghafi (GDP) la katika kaunti hiyo na kuwahimiza vijana kuchangamkia fursa zilizopo ndani ya maeneo yao.
“Nchi iko katika mwelekeo sahihi,” alisema, akiwashauri vijana kutotafuta mafanikio mbali bali kubuni, kulima, kuzalisha na kujenga ndani ya jamii zao.
Mojawapo ya matukio muhimu katika mkutano huo ilikuwa ni uzinduzi wa mifumo ya ufadhili inayoungwa mkono na serikali kwa ajili ya wafanyabiashara na wajasiriamali katika sekta mbalimbali kama kilimo, viwanda, afya, hoteli, TEHAMA na uvumbuzi.
Washiriki walihimizwa kutumia taasisi kama vile: Shirika la Maendeleo la Kenya (KDC) – hutoa mikopo ya kati ya KSh milioni 10 hadi KSh milioni 250 kwa riba ya 12%, inayolipwa ndani ya miaka 5 hadi 7.

Mashirika ya Viwanda ya Kenya (KIE) – hutoa mikopo ya kati ya shilingi milioni 1 hadi milioni 20 kwa riba ya 10%, pia inayolipwa kwa muda mrefu.
Mamlaka ya Uwekezaji Kenya (KenInvest) – huunganisha wafanyabiashara na wawekezaji wa kimataifa kusaidia upanuzi na ufadhili.
Tofauti na benki za kibiashara ambazo hutoza viwango vya riba vya juu hadi 18%, mashirika haya ya serikali yanatoa njia nafuu na rahisi za kifedha kwa kampuni zinazochipukia, wakulima, biashara ndogo na za kati (SMEs), na miradi inayoongozwa na vijana.
Mkutano huo haukuhusu tu masuala ya kifedha. Ulileta mijadala yenye maana kuhusu uongezaji thamani katika kilimo, uendelezaji wa mifugo, utalii, ubunifu wa kidijitali, na uzalishaji wa viwandani — yote yakiwa yamewekwa ndani ya maono ya maendeleo jumuishi na endelevu ya kaunti.
Washirika wa ndani kama Credible Brooms, Chama cha Hifadhi za Laikipia, GROOTS Kenya, Benki ya Ushirika, na Ujuzi na Biashara walichangia kwa kiasi kikubwa kwenye mazungumzo haya, wakithibitisha kuwa ushirikiano ni msingi wa ukuaji wa maana.

Waziri wa Uwekezaji, Biashara na Viwanda, Lee Kinyanjui, alisisitiza dhamira ya serikali kuu katika kusambaza maendeleo ya kiuchumi hadi ngazi za kaunti kupitia majukwaa ya uwekezaji.

Alieleza kuwa majukwaa haya yataongeza biashara za ndani na za kikanda huku yakichangamkia fursa zilizopo katika mikataba ya kibiashara ya kimataifa na EU, Uingereza, UAE na China.
“Tunaendelea kushirikiana na mashirika kama KenInvest na KDC ili kupanua upatikanaji wa mitaji kwa SMEs na kuimarisha uhusiano wa masoko,” alisema Waziri Kinyanjui.
Naibu Gavana wa Laikipia, Reuben Kamuri, aliongeza kuwa serikali ya kaunti inaendelea kuboresha mazingira ya uwekezaji kupitia ushirikiano, motisha kwa wawekezaji, na sera madhubuti za kusaidia ukuaji wa uchumi.
Kadri kaunti ya Laikipia inavyotazamia siku za usoni, ujumbe ni mmoja: kuna fursa kubwa katika uwekezaji unaoanzia mashinani, na vijana ndio wanaopaswa kuwa mstari wa mbele. Kupitia ufikiaji rahisi wa rasilimali fedha, usaidizi wa kitaasisi, na masoko yanayoendelea kupanuka, Laikipia inajitokeza kuwa mfano bora wa kile kaunti za Kenya zinaweza kufanikisha kwa mipango jumuishi ya kiuchumi.
.