Konstebo wa polisi Klinzy Barasa Masinde alifikishwa mahakamani leo Jumatatu na kukanusha mashtaka ya kumuua mchuuzi wa barakoa Boniface Kariuki.
Masinde anatuhumiwa kwa kumfyatulia risasi Kariuki wakati wa maandamano ya kulalamikia mauaji ya mwanablogu na mwalimu Albert Ojwang Juni 17 mwaka huu.
Mchuuzi huyo alifariki baadaye wakati akipokea matibabu katika Hospitali ya Kitaifa ya Rufaa ya Kenyatta, KNH.
Juhudi za mawakili wa mshukiwa huyo za kutaka aachiliwe huru kwa dhamana ziliambulia patupu baada ya Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (DPP) kuzipinga vikali.
Awali, DPP Renson Ingonga aliidhinisha mashtaka ya mauaji dhidi ya afisa huyo wa polisi.
Masinde sasa atasalia korokoroni hadi Agosti 19 wakati ombi la kutaka aachiliwe kwa dhamana litakaposikilizwa.