Koimburi hakutekwa nyara, imesema Huduma ya Taifa ya Polisi

Tom Mathinji
2 Min Read
Mbunge wa Juja George Koimburi.

Huduma ya Taifa ya Polisi imebainisha kuwa mbunge wa Juja George Koimburi, alisingizia kuwa ametekwa nyara ili apate umaarufu wa kisiasa.

Wakiwahutubia wanahabari kwa pamoja, Inspekta Jenerali wa Polisi Douglas Kanja na Mkurugenzi wa Idara ya Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI) Mohamed Amin, walisema utekaji nyara huo bandia ulihusisha wandani wa mbunge huyo.

Kulingana na maafisa hao, washukiwa wengine watatu walikamatwa na kutoa habari za kina kuhusu jinsi utekaji nyara huo bandia ulivyotekelezwa.

“Washukiwa wengine watatu, Peter Kiratu ambaye ni mwenyekiti wa Hazina ya Maendeleo ya Maeneo bunge (NG-CGF), Cyrus Kieru na Karanja Gatana walikamatwa na kutoa habari kwa polisi ambazo zimeelezea zaidi kuhusu madai hayo ya utekaji nyara,” alisema Kanja.

Kulingana na  Kanja, Karanja Gatana aliwaambia polisi kwamba walimsaidia Koimburi kurarua mavazi yake, ili kughushi ushahidi wa kudhulumiwa, huku Peter Kiratu ambaye njama hiyo ilipangiwa nyumbani kwake,  akiwa mshauri mkuu wa njama hiyo.

Washukiwa hao watatu pia waliweza kutambua gari aina ya Subaru iliyotumika kumteka nyara mbunge huyo.

Muhia, ambaye anamiliki duka la jumla katika mtaa wa Kahawa West, alisema kuwa alipokea simu kutoka kwa Kiratu Mei 24, 2025, akimwitisha gari lake aina ya Subaru ili itumike kuwabeba maafisa zaidi wa usalama wakati mbunge huyo atakapokuwa akihudhuria ibada ya Jumapili.

Mnamo Mei 25, 2025,Kiratu alimwagiza Muhia kuenda nyumbani kwake Mugutha, alikokutana na Gatana aliyekuwa akiendesha gari la Kiratu aina ya Honda CRV, akiwa na wanaume wengine watatu.

Baada ya utekaji nyara huo bandia, polisi wanasema gari hilo liliendeshwa hadi katika Taasisi ya Utafiti wa Kahawa kupitia barabara ya kambogo, kabla ya kuamrishwa na mbunge huyo kusimama kando ya gari la Kiratu  Honda CRV.

Maafisa hao walisema uchunguzi unaendelea na kwamaba wamefuatilia mienendo ya mbunge huyo kutoka kanisani hadi katika shamba la kahawa alikopatikana.

Wameapa kumchukulia hatua za kisheria mbunge huyo, punde tu uchunguzi utakamilika.

Share This Article