Koffi Olomide apeleka burudani nchini Uganda

Yeye ni mgeni rasmi katika tamasha la kuadhimisha miaka 50 ya bendi ya Afrigo Jumamosi Agosti 16, 2025 .

Marion Bosire
2 Min Read

Mwanamuziki maarufu wa Congo Koffi Olomide yuko nchini Uganda ambapo anatarajiwa kuburudisha mashabiki zake na wale wa bendi ya Afrigo.

Koffi ndiye mgeni rasmi katika tamasha la kuadhimisha miaka 50 ya bendi hiyo ya Afrigo litakaloandaliwa Jumamosi Agosti 16, 2025 katika uwanja wa Millenium, Lugogo jijini Kampala nchini Uganda.

Bendi hiyo yenye wanachama kama Moses Matovu, Rachel Magoola, Joanita Kawalya, Herbert Kigundu, Sarah Namulondo, Charles Busuulwa na wengine ilibuniwa mwaka 1975.

Tangu wakati huo imekuwa ikitoa burudani kwa raia wa Uganda na hata mashabiki wa ughaibuni kwa kujumuisha mitindo ya kitamaduni na ya kisasa.

Kampuni ya Talent Africa Group ndiyo inaandaa tamasha hilo chini ya msururu wa matamasha uliopatiwa jina la The Legends of Sound kwa lengo la kutambua magwiji wa muziki barani Afrika.

Afisa mkuu mtendaji wa kampuni hiyo Aly Allibhai anaahidi tamasha la kufana siku hiyo watakapokuwa wakisherekea waimbaji hao wa muda mrefu nchini Uganda kwa ushirikiano na benki ya Stanbic.

Wanachama waanzilishi wa bendi hiyo ni pamoja na Moses Matovu, Charles Ssekyanzi, Jeff Sewava, Paddy Nsubuga, Paulo Serumagga, Fred Luyombya, Anthony Kyeyune na Geoffrey Kizito.

Kufikia mwaka 2015 wote walikuwa wameshaaga dunia isipokuwa Moses Matovu ambaye sasa ana umri wa miaka 76 na anahudumu kama kiongozi wa bendi.

Kadri miaka ilivyosonga wasanii wengine wengi walijiunga na bendi hiyo wakiwemo wacheza densi wa kike.

Share This Article