KNH yasema afya ya pacha walioungana ni imara

Watoto hao waliozaliwa siku chache huko Naivasha walihamishiwa KNH ambapo matatizo yao ya kiafya yanaendelea kushughulikiwa.

Marion Bosire
1 Min Read

Hospitali ya Kitaifa ya Rufaa ya Kenyatta – KNH imeripoti kwamba imefanikiwa kuimarisha afya ya pacha walioungana waliozaliwa mjini Naivasha na hivyo kuipa familia yao matumaini.

Pacha hao walizaliwa kwa njia ya upasuaji katika hospitali ya kaunti huko Naivasha Agosti 13, 2025, wakiwa na uzani wa pamoja wa kilo 3.6.

Walipatiwa rufaa ya haraka hadi hospitali ya kitaifa ya Kenyatta mapema Agosti 14, 2025 na walipofikishwa huko na kufanyiwa ukaguzi, ilionekana kwamba wameunganika kwenye tumbo na nyonga.

Walipatikana pia kuwa na tatizo la kukosa sehemu ya kupitisha choo hali iliyohitaji upasuaji wa haraka.

Agosti 17, watoto hao walifanyiwa upasuaji na kundi la madaktari wenye ujuzi na hivyo kutengeneza njia hiyo muhimu ya kupitisha choo, hali iliyoimarisha afya yao na hivyo kutoa fursa kwa matibabu zaidi.

Pacha hao wana utumbo mkubwa mmoja, wote wawili wana matatizo kwenye roho zao, maini yao yana matatizo na damu yao imeathirika, matatizo ambayo yanaendelea kushughulikiwa na madaktari wenye ujuzi mbalimbali.

Hospitali ya Kenyatta kupitia kwa Dkt. Evanson Kamuri inahakikishia umma kwamba itaendelea kusaidia familia ya watoto hao katika safari yao ya matibabu.

Share This Article