KNH yalalamikia ongezeko la idadi ya wagonjwa

Ongezeko hilo limehusishwa na migomo inayoendelea ya wahudumu wa afya katika kaunti za Nairobi na Kiambu, migomo ambayo imeathiri mno utoaji wa huduma za afya katika kaunti hizo.

Martin Mwanje
2 Min Read

Hospitali ya Kitaifa ya Rufaa ya Kenyatta, KNH imelalamikia ongezeko la wagonjwa wanaotafuta huduma za matibabu hospitalini hapo. 

Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa hospitali hiyo Dkt. Richard Lesiyampe amehusisha ongezeko hilo na migomo ya wahudumu wa afya inayoendelea katika kaunti za Nairobi na Kiambu.

“Hospitali ya Kitaifa ya Rufaa ya Kenyatta inashuhudia ongezeko la wagonjwa wanaotafuta huduma za matibabu, kufuatia mgomo unaoendelea wa wahudumu wa afya katika kaunti za Kiambu na Nairobi, alisema Dkt. Lesiyampe kwenye taarifa.

“Huku hospitali nyingi za umma katika kaunti hizo mbili zikiwa hazihudumu kikamilifu, KNH imekuwa kituo kikuu cha kuwahudumia wagonjwa wanaohitaji matibabu ya dharura.”

Dkt. Lesiyampe akilalamika kuwa baadhi ya kina na watoto wanawasili hospitalini humo kuchelewa na wachache kupoteza maisha licha ya matabibu kufanya kila wawezalo kuokoa maisha yao.

Kulinga naye, ongezeko la wagonjwa hospitalini hapo pia limekuwa mzigo kwa utoaji huduma muhimu za matibabu kama vile vyumba vya upasuaji na hifadhi ya damu.

“Wafanyakazi wetu wanafanya kazi kadiri wawezavyo saa 24, lakini kuna uhaba wa rasilimali,” aliongeza Dkt. Lesiyampe.

Ni hali ambayo imemfanya kutoa wito kwa pande zinazovutana katika kaunti za Kiambu na Nairobi kusuluhisha tofauti zao ili huduma za matibabu zirejee kama kawaida.

Jana Jumanne, kaunti ya Murang’a pia ililalamikia ongezeko la wagonjwa wanaotafuta huduma za matibabu katika kaunti hiyo, yamkini kutoka kaunti jirani ya Kiambu.

Ingawa baadhi ya wabunge katika kaunti ya Kiambu wamelalamikia kuzorota kwa huduma za matibabu katika kaunti hiyo, Gavana Kimani Wamatangi amepuuzilia mbali malalamiko yao akiyataja kuwa porojo za kisiasa.

 

Share This Article