KMPDU yatishia kuhamasisha wanachama wake kugoma

Marion Bosire
1 Min Read

Chama cha madaktari, wanafamasia na wataalamu wa meno nchini KMPDU kimetishia kuhamasisha wanachama wake wote kote nchini kushiriki mgomo na maandamano kuunga mkono wezao wa kaunti ya Kiambu.

KMPDU inalaumu usimamizi wa serikali ya kaunti ya Kiambu kwa kushindwa kusimamia mgomo huo ambao sasa umedumu zaidi ya siku 128.

Katika taarifa, katibu mkuu wa chama cha KMPDU Dkt. Davji Atellah alilaumu utawala wa Gavana Kimani Wamatangi wa kususia makubaliano ya kurejea kazini yaliyotiwa saini mwaka jana.

Atellah alilaumu serikali ya Wamatangi pia kwa kutelekeza maslahi ya wananchi ambao wamekuwa wakisumbuka na kukosa huduma za afya kufuatia mgomo huo.

Chama hicho kimetangaza mipango ya kutekeleza maandamano kwa pamoja na familia zilizoathiriwa na mzozo huo wa sekta ya afya, wakiwemo kina mama waliopoteza wanao wachanga.

Kulingana na KMPDU, huo ndio utakuwa mwanzo wa kampeni ya kitaifa ya sekta ya afya iwapo serikali ya kaunti ya Kiambu haitachukua hatua mwafaka.

Wakati huo huo, Gavana Wamatangi ameshikilia kwamba kamwe hatowalipa madaktari wanaogoma akisisitiza kwamba ni lazima kwanza warejee kazini.

Msimamo huo wa Gavana wa Kiambu umetajwa na KMPDU kuwa hatua inayokoleza mzozo wa sekta ya afya katika kaunti hiyo.

Share This Article