Kivumbi kinatarajiwa kutifuliwa kesho Jumamosi wakati ambapo kongamano la 38 la Umoja wa Afrika (AU) litapiga kura kubaini mwenyekiti mpya wa tume ya Umoja wa Afrika (AUC).
Marais na viongozi 49 watashiriki zoezi hilo muhimu huku mshindi kati ya wawaniaji watatu wa kiti hicho, Raila Odinga wa Kenya, Richard Randriamandrato wa Madagascar na Mahamoud Yousouf kutoka Djibouti akitarajiwa kubainika.
Mataifa mengine ya Burkina Faso, Mali, Guinea, Niger, Gabon na Sudan, hayatapiga kura baada ya kupigwa marufuku kutokana na mapinduzi ya serikali na wanajeshi.
Ili kutangazwa mshindi, Raila anahitaji kupata kura 33 katika raundi ya kwanza ya upigaji kura itakayoanza kesho.
Endapo hakuna mwaniaji atakayepata ushindi katika raundi ya kwanza, upigaji kura utaingia raundi ya pili ambapo mwaniaji wa mwisho katika raundi ya kwanza ataondolewa kwenye debe.
Raundi ya tatu ya upigaji kura itahitajika ikiwa hakutakuwa na mshindi atakayepata theluthi mbili ya kura kwenye raundi ya pili, mgombeaji atakayemaliza wa pili akiondolewa.
Mwaniaji atakayeongoza raundi ya pili pekee atashirikishwa katika raundi ya tatu ya upigaji kura.
Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC), ina jumla ya kura 16 huku mataifa mengi yakitarajiwa kumuunga mkono mgombeaji wa Madagascar.
Raila kwa upande wake anatarajiwa kupata uungwaji mkubwa kutoka kwa mataifa manane ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), huku Yousouf akilenga kupata uungwaji mkono kutoka kwa baadhi ya nchi wanachama wa IGAD.
Kando na miungano ya kiuchumi, huenda mataifa hayo 49 yakapiga kura kwa kuzingatia ushirikiano wa kidiplomasia na nchi zilizo na wawaniaji.
Mwenyekiti mpya atamrithi Moussa Faki wa Chad ambaye amehudumu tangu mwaka 2017.
Raila amezuru takriban mataifa yote 49 ya Afrika katika juhudi za kutafuta uungwaji mkono, zoezi ambalo limepigwa jeki na serikali ya Kenya.