Faith Kipyegon amenyakua nishani ya nne ya dhahabu ya dunia katika mbio za mita 1500 na ya tatu mtawalia leo jioni mjini Tokyo, Japan.
Kipyegon ameziparakasa mbio hizo kwa muda wa dakika 3 sekunde 52.15, huku Dorcas Ewoi aliyekuwa akishiriki mashindano ya Dunia kwa mara ya kwanza akinyakua fedha kwa dakika 3 sekunde 54.94.
Jessica Hull wa Australia ameshinda shaba kwa muda wa dakika 3 sekunde 55.15, naye Nelly Chepchirchir wa Kenya akaridhia nafasi ya nne.
Bingwa huyo mara tatu wa Olimpiki ndiye mwanariadha wa kwanza kunyakua dhahabu nne za dunia mwaka 2017, 2022, 2023 na mwaka huu.
Kenya ingali ya pili kwenye msimamo wa dunia baada ya kuzoa dhahabu 3, fedha 1 na shaba 1.
Marekani inaongoza msimamo wa dunia kwa dhahabu 6 na shaba 2.