Kindumbwendumbwe cha kuwania kombe la bara Afrika kwa chipukizi wasiozidi umri wa miaka 20, kitaingia hatua ya nusu fainali leo nchini Misri, huku timu zote zilizosalia zikiwa tayari zimefuzu kwa fainali za Kombe la Dunia.
Nigeria wanaojivunia kutwaa kombe hilo mara saba, watashuka dimbani 30th June jijini Cairo, kuanzia saa kumi na mbili jioni kukabana koo na Afrika Kusini, kabla ya kupisha derby ya kaskazini mwa Afrika kati ya wenyeji Misri na Morocco, kuanzia mida ya saa tatu usiku.
Nigeria iliwatema nje mabingwa watetezi Senegal, kupitia penati 3-1, kufuatia sare kappa katika robo fainali, huku Afrika Kusini ikiwazidia maarifa Jamhuri ya Demokrasia ya Congo, bao moja kwa nunge katika muda wa ziada baada ya kutoka sare tasa.
Morocco walihitaji bao la muda wa ziada ili kuwashinda Sierra Leone, goli moja bila jibu katika robo fainali huku Misri ikiwabandua Ghana penati 5-4 kufuatia sare ya 2-2.
Fainali ya kipute hicho itasakatwa Jumapili hii, Mei 18.