Serikali imejitolea kuhakikisha vizingiti vinavyohujumu upatikanaji wa vitambulisho hasaa miongoni mwa vijana, vinaondolewa.
Katibu wa idara ya Uhamiaji na Huduma kwa Wakenya Dkt. Belio Kipsang, alisema upatikanaji wa vitambulisho na vyeti vya kuzaliwa sio tu haki ya kikatiba lakini pia hufanikisha ushirikishwaji katika uchumi wa kijamii.
“Tumejitolea kuondoa vizingiti vyote vinavyohujumu vijana kupata stakabadhi hiyo muhimu,” alisema Kipsang.
Kipsang aliyasema hayo Ijumaa wakati wa hafla ya uhamasishaji jamii kwenye kaunti ndogo ya Tinderet, kaunti ya Nandi.
“Upatikanaji wa vitambulisho sio tu haki ya kikatiba lakini pia ni stakabadhi muhimu kwa vijana wetu wanaotafuta elimu ya juu, ajira au huduma za serikali,” alisema Kipsang.
Hafla hiyo ilitoa fursa kwa umma kutangamana na huduma zinazotolewa na serikali.