Aliyekuwa Waziri Mkuu wa Kenya Raila Odinga, ameaga dunia, akipokea matibabu nchini India.
Kiongozi huyo wa chama cha Orange Democratic Movement (ODM), amefariki Jumatano katika mji wa Kochi, baada ya kuugua kile kinachoaminika kuwa mshtuko wa moyo alipokuwa akitembea katika hospitali ya macho ya utafiti wa Sreedhareeyam Ayurvedic.
Raila amekuwa akipokea matibabu nchini India kwa muda wa siku tano zilizopita, huku hali yake ya kiafya ikiibua hisia mseto hapa nchini.
Iliripotiwa kuwa Raila alipata matatizo ya kupumua na kuzimia mwendo wa saa mbili asubuhi.
Alipelekwa katika hospitali ya kibinafsi iliyo karibu, lakini hali yake ikadhoofika. Raila alikuwa matembezini na dada yake, binti yake Rosemary na daktari wa kibinafsi alipozirai.
Familia yake awali ilisisitiza kuwa Raila alikuwa katika hali nzuri ya kiafya, na kwamba alikuwa akipokea matibabu.
Raila Odinga alizaliwa Januari 7, 1945, Maseno, akiwa mwana wa Mary Odinga na Jaramogi Oginga Odinga aliyekuwa Makamu Rais wa kwanza wa Kenya.