Kenya imeilaumu Tanzania kutokana na hatua yake ya kuwazuia raia wa kigeni kufanya baadhi ya biashara nchini humo.
Waziri wa Biashara na Ustawi wa Viwanda Lee Kinyanjui, alisema hatua hiyo ya Tanzania ambayo ni mwanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, inakiuka maudhui ya kanda hiyo.
Kinyanjui alisema hatua zilizochukuliwa na Tanzania, zinahujumu lengo la utangamano wa kiuchumi chini ya itifaki ya soko la pamoja (CMP).
“Sehemu ya 13 ya Itifaki ya Soko la Pamoja, inaruhusu raia wa mataifa ya EAC kuanzisha na kufanya biashara, bila kupendelea raia wa taifa husika dhidi ya wale wa Afrika Mashariki. Kenya inapendekeza kuondolewa kwa vikwazo hivyo na Tanzania irejelee masharti yaliyo katika itifaki ya EAC,” alisema Kinyanjui kupitia kwa taarifa.
Kwa sasa takriban raia nusu milioni wa Kenya wanaanya biashara au wameajiriwa nchini Tanzania.
Kulingana na Kinyanjui, Jumuiya ya EAC inasalia kuwa soko kubwa la bidhaa za Kenya, huku ikiuza asilimia 28.1 ya bidhaa za Kenya zinazouzwa nje, zikikadiriwa kuwa shilingi bilioni 297 mwaka jana.
Wakati huo huo Kenya imeibua wasiwasi kuhusu hatua ya hivi majuzi iliyochukuliwa na Tanzania ya Mswada wa Fedha wa mwaka 2025 na sheria ya Tanzania ya ushuru iliyofanyiwa marekebisho ya mwaka 2019, ambazo zimebuni ushuru wa maendeleo wa asilimia 10 na 15 mtawalia.
Kinyanjui alisema utozaji ushuru kwa mapendeleo, unahatarisha kusambaratisha ufanisi wa kibiashara ulioafikiwa.
“Kenya inatambua uhuru wa mataifa wanachanama wa EAC kubuni maswala ya ndani, lakini pia inaamini kuhusu umuhimu wa mashauriano, ushirikiano na utekelezwaji wa sera zinazoathiri usafiri wa bidhaa mipakani,” aliongeza Kinyanjui.
Sasa Kenya, inatafuta mashauriano ya pande mbili, ili kutatua swala hilo.